NA GODFREY NNKO
KAMISHNA wa Mamlaka ya Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA),Mabula Misungwi amesema, mamlaka hiyo imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 184.74 katika kipindi cha kati ya mwaka 2020/21 hadi Machi, 2024.
Akifafanua kuhusu ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka amesema, mwaka 2020/21 maduhuli ya jumla kupitia vyanzo mbalimbali yalikuwa shilingi bilioni 25.75 huku mwaka 2021/22 makusanyo yakifikia shilingi bilioni 49.54.
Kamishna Mabula ameendelea kufafanua kuwa, kwa mwaka 2022/23 makusanyo yalikuwa shilingi bilioni 55.57 ambapo kwa mwaka 2023/24 katika kipindi cha Julai hadi Machi 15 makusanyo yamefikia shilingi bilioni 53.87.
"Tumeimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya jumla kupitia vyanzo mbalimbali na kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali kiasi cha shilingi bilioni 184.74 kati ya mwaka 2020/21 hadi Machi, 2024."
Ameyasema hayo leo Machi 18, 2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Leo, TAWA ilikuwa taasisi ya 58 kukutanishwa na wahariri ili kuelezea ilipotoka, ilipo, inapoelekea na mafanikio yake ikiwa ni utaratibu uliowekwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ili umma uweze kufahamu kuhusu maendeleo ya mashirika na taasisi zao.
Kamishna Mabula amesema, hayo ni sehemu ya mafanikio ya TAWA kwa kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Wakati huo huo,Kamishna Mabula amesema, kwa kutumia fedha zilizotolewa kwa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 (Tanzania Social Economic Response and Recovery Plan-TCRP ) miundombinu wezeshi ya utalii katika maeneo yanayosimamiwa na mamlaka imeboreshwa
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na kujenga kwa kilomita 431.4 za barabara katika Mapori ya Wamimbiki, Mpanga Kipengere, Igombe, Swagaswaga, Mkungunero, Kijereshi, Rungwa na Pande,
Pia, amesema wamefanikiwa kufanya ukarabati wa viwanja vya ndege vitatu katika Pori Tengefu Lake Natron (Engaresero) na Pori la Akiba Maswa (Buturi na Mbono).
"Na kujenga miundombinu ya kupumzika wageni (Bandas 13, Campsites - 6, picnic sites - 8, lounge 1) na hosteli moja katika Mapori ya Akiba Mpanga Kipengere, Mkungunero, Lukwika Lumesule, Pande Swagaswaga na Magofu ya Kilwa,"
Ameongeza kuwa, kupitia fedha hizo wamejenga malango matano na vituo vinne vya kukusanyia mapato katika Mapori ya Akiba ya Wamimbiki, Mkungunero, Lukwika Lumesule, Swagaswaga, Mpanga Kipengere, Kijereshi na katika Pori Tengefu Lake Natron,
Mradi mwingine ni ujenzi wa njia ya waenda kwa miguu zenye urefu wa kilometa 3.7 katika Pori Tengefu Ziwa Natron, na Mapori ya Akiba Swagaswaga, Kilwa Kisiwani na Mpanga Kipengere,
Sambamba na ukarabati wa mabanda sita ya Utalii katika Pori la Akiba Wamimbiki. "Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutuamini na kutupatia fedha za kuboresha miundombinu hii ya utalii."
Kamishna Mabula amesema, pamoja na kuboresha miundombinu ya uhifadhi na utalii, TAWA ilijielekeza pia kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuongeza ufanisi utendaji kazi.
Amesema, kupitia bajeti ya Mamlaka ya Maendeleo na fedha zilizotolewa kwa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 (Tanzania Social Economic Response and Recovery Plan (TCRP ) TAWA imefanikiwa kujenga maghala ya silaha 25.
Kamisha Mabula amesema, pia wamejenga nyumba za watumishi 26, vituo 28 vya askari (rangers Posts) na ofisi 10 na Karakana nne ili kuboresha mazingira ya utendaji kazi.
"Vilevile Mamlaka imenunua vitendea kazi ikiwemo magari 60,boti za doria saba na utalii mbili zenye uwezo wa kubeba abiria 30 na 60, mahema, sare za watumishi, mtambo wa kuchimba visima na gari la kubeba mitambo.
"Na tumenunua mtambo wa barabara (grader), silaha,kuweka mifumo ya mawasiliano, radio za upepo,mfumo wa kukusanya taarifa za doria (Smart na GPS),"amefafanua Kamishna Mabula.
Mbali na hayo, Kamishna Mabula amesema, mamlaka imejiimarisha katika matumizi ya mifumo ya Teknolojia na Mawasiliano (TEHAMA) katika ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo wa MNRT Portal, uandaaji wa bajeti (PlanRep).
Pia, matumizi (MUSE), kushughulikia majadala e-office, huduma kwa wateja (chatroom) na mfumo wa kukusanya taarifa za uhifadhi (Conservation Information System) na mfumo wa kukusanya taarifa za doria (Special Monitoring AR Tool)
"TAWA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maelekezo ya viongozi mbalimbali wa wizara na Kitaifa.
"Pia, tutaendelea kuongeza ubunifu na mbinu mbalimbali kukabiliana na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu,ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na kuongeza mapato pamoja na kushirikiana na wadau na kushiriki katika majukwaa ya Kimataifa kuelezea faida za uwindaji wa kitalii ili kukabiliana na kampeni za kupinga uwindaji.
"Ili kutekeleza azma hii muhimu kwa Serikali, mamlaka inaongeza nguvu katika matumizi ya teknolojia katika ulinzi na usimamizi wa mapato ya Serikali,"amefafanua Kamishna Mabula.
Tags
Habari
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF)
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA)
Ofisi ya Msajili wa Hazina
TAWA
TAWA Tanzania