TAWA yatoa gawio kwa halmashauri 32,vijiji 187

NA GODFREY NNKO

KAMISHNA wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Management Authority-TAWA),Mabula Misungwi amesema, kutokana na shughuli za utalii wa picha na uwindaji wamekuwa wakitoa gawio kwa halmashauri za wilaya 32 na vijiji 187.
Ameyasema hayo leo Machi 18, 2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

TAWA ambayo ipo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ilianzishwa kwa mujibu wa Kifungu cha 8 cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya Mwaka 2009 na kutangazwa kwa amri (Order) ya Serikali iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 135 la tarehe 09 Mei 2014, pamoja na marekebisho yaliyochapishwa katika gazeti la Serikali Na. 20 la tarehe 23 Januari 2015.

Aidha, mamlaka hiyo ambayo inasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ilianza kazi rasmi tarehe 1 Julai 2016 kwa kuchukua majukumu ya kiutendaji ya Idara ya Wanyamapori kuhusu usimamizi wa rasilimali ya wanyamapori nje ya Hifadhi za Taifa na Hifadhi ya Ngorongoro.

"Katika kipindi cha mwaka 2021/22 - 2023/24 jumla ya shilingi Bilioni 8.95 zilitolewa kwa wanufaika. Pamoja na kuimarisha mahusiano na dhana nzima ya uhifadhi kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi, fedha hizo zinatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayoibuliwa na wananchi,"amesema Kamishna Mabula.

Pia amesema, mamlaka imekuwa ikisimamia na kurejesha stahili zinazotokana na shughuli za utalii katika maeneo ya Jumuiya za Uhifadhi za Wanyamapori.
Kamishna Mabula amefafanua kuwa, kati ya mwaka 2021-2024 jumla ya shilingi Bilioni 11.91 zilirejeshwa kwa Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori 13 kwa ajili ya kuendeleza uhifadhi na miradi ya maendeleo kwa vijiji vilivyotoa ardhi yao kuwa hifadhi za wanyapori.

"Kufuatia juhudi za Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutangaza utalii kupitia Filamu ya the Royal Tour, kutoa fedha za kuendeleza miundombinu ya utalii na fursa za kutangaza katika masoko ya Kitaifa na Kimataifa mafanikio lukuki yamepatikana."

Amesema, mafanikio hayo ni idadi ya watalii wa picha na uwindaji imeendela kuongezeka. "Idadi ya watalii wa picha waliotembelea vivutio kutoka 37,684 mwaka 2020/21 hadi 166,964 mwaka 2022/23 na watalii 116,529 hadi Februari 2024.

"Wawindaji kutoka 355 mwaka 2020/21 hadi wawindaji 787 mwaka 2022/23 na wawindaji 481 hadi Februari mwaka 2024."

Kamishana Mabula amesema, pia kuna ongezeko la idadi za meli za Kimataifa za utalii ambao wanatembelea Eneo la Kihistoria Kilwa kutoka meli nne zilizokuwa na watalii 400 mwaka 2020/21 hadi meli 8 zenye watalii 925.

"Na kuuza vitalu kwa Mnada wa Kieletroniki na kuanza utekelezaji wa Uwekezaji Mahiri. "Miongoni mwa matunda ya Filamu ya Royal Tour ni mwitikio wa mkubwa wa wawekezaji katika mnada wa vitalu vya utalii ambapo jumla ya vitalu 66 vimeuzwa na mapato ya jumla ya Dola za Kimarekani 8,277,000 zilikusanywa.

"Hiyo ni ikilinganishwa na Dola 2,405,000 endapo vitalu hivyo vingeuzwa kwa njia ya utawala ikiwa ni ongezeko la Dola 5,872,000."
Amesema,Serikali imekamilisha taratibu za uwekezaji kwa ajili ya kusaini mikataba ya uwekezaji mahiri katika Vitalu vya Ikorongo, Grumeti, Maswa Mbono, Maswa Kimani, Maswa North, Mkungunero na Selous LL1.

"Mikataba saba ilisainiwa Januari 2024 ambapo kupitia mikataba hiyo Serikali itapata Dola za Marekani milioni 312. 25 kwa kipindi cha miaka 20 sawa na wastai wa Dola za Marekani milioni 15.5."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news