NA FRESHA KINASA
RAIS wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA),Vicent Minja amempongeza Mkurugenzi wa Kiwanda cha Mafuta ya Alzeti cha Nyihita Sunflower Cooking Oil Production kilichopo Nyanchabakenye Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Wilfred Nyihita.
Ni kwa hatua yake ya kuingia kwenye kilimo cha zao hilo, hatua ambayo itasaidia kukifanya kilimo hicho kikue na hivyo kuongeza uzalishaji wa mafuta nchini.
Wilfred Nyihita kwa sasa ameamua kuanzisha shamba la alzeti la Nyihita Agro Consultancy and Sunflower Oil Mill lenye ukubwa wa hekta 85 lililopo Kirumi Wilaya ya Butiama kutokana na wakulima kushindwa kuzalisha alzeti kwa wingi ili kukidhi mahitaji ya kiwanda chake.
Minja amesema kuwa, uwekezaji huo unasaidia kuifanya sekta binafsi kuwa na mchango wa maendeleo ya ukuzaji wa uchumi na kuendana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita kuona sekta binafsi inachochea uchumi na kuleta mageuzi chanya.
Ameyasema hayo leo Machi 22, 2024 alipotembelea mradi wa shamba hilo wilayani Butiama pamoja na kiwanda cha alzeti kilichopo Nyanchabakenye Wilaya ya Rorya mkoani humo.
Amesema kuwa, Nyihita anafanya kazi kubwa na nzuri ambayo inapaswa kupongezwa, kwani mchango wake katika maendeleo ni mkubwa.
Hivyo, TCCIA itaendelea kumpa ushirikiano wote na kumuunganisha na fursa kubwa za kupanua uwekezaji huo. Ambapo amewahimiza wakulima Mkoa wa Mara kulima kwa uhakika zao hilo kutokana na uhakika wa soko.
Ameongeza kuwa, ni faraja kubwa kuona Nyihita ameonesha uthubutu na uhodari kwa kujenga kiwanda hicho na kuanzisha shamba kubwa hatua ambayo itasaidia ajira, soko la zao hilo na elimu kwa wakulima wanaotaka kuzalisha alizeti kwa tija ili wakue kiuchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Nyihiya Agro Consultancy and Sunflower Oil Mills, Wilfred Nyihita amesema kuwa, taasisi hiyo inajishughulisha na kilimo cha zao la alzeti na kiwanda cha kukamua mafuta ya mbegu za alzeti.
Amesema, malengo ya mradi huo ni kuwa na shamba kubwa la uzalishaji wa zao la alzeti la mfano kwa ajili ya kutosheleza kiwanda kilipo Kijiji Cha Nyanchabakenye Wilaya ya Rorya, kutoa kituo cha mafunzo kwa wanafunzi wa vyuo kutoa elimu pamoja na wakulima kujifunza kanuni bora za kilimo cha alzeti.
Pia amesema kuchangia na kupunguza uhaba wa mafuta hapa nchini, kuchangia pato la nchi kwa kulipa kodi, kutengeneza ajira n kufanya matumizi bora ya ardhi kwa mujibu wa sera ya nchi na sheria.
Amebainisha kuwa, mradi huo wa shamba umeanza Januari 29, 2024 na umetekelezwa katika hatua ikiwemo kusafisha shamba la mradi ambalo haijawahi kutumika kwa asilimia 99, kwani ilikuwa na vichaka vizito.
Pia upimaji wa shamba kwa kutumia wataalamu wa kilimo, ili kuweza kupima shamba na kugawa vitalu ambapo kila kitalu kina ukubwa wa hekta moja sawa na hekari mbili na nusu.
Amesema, shughuli ya uchongaji wa barabara pia imefanyika kusaidia shamba kupitika kirahisi bila kuathiri mazao na kuzuia maambukizi ya magonjwa ya mazao kutoka kitalu kimoja kwenda kingine na kusaidia kukinga majanga kama moto na kurahisisha mfumo wa umwagiliaji mazao shambani.
"Tumeweza kulima shamba lote la mradi kwa kutumia zana za kitaalamu kwa ajili ya kurahisisha ulimaji wa shamba ambazo ni trekta.
"Pia baada ya kulima shamba hadi sasa zoezi la upandaji mbegu za alzeti linaendelea tunatumia zana za kitaalamu na aina ya mbegu tunazopanda ni Hysun na eneo lilopandwa hadi sasa ni hekta 85 hekari 15 mbegu za mahindi na hekali 70 zimepandwa alizeti.
"Kwa sasa tunalima tukiwa tunategemea mvua ili kuzalisha, lakini mpango wetu wa baadaye ni kufunga mifumo ya umwagiliaji inayotumia nguvu ya umeme kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
"Na matarajio ya mavuno ya zao hili la alzeti katika msimu huu wa kilimo ni tani 121 iwapo msimu utakuwa mzuri ambapo tani hizo 121 zinatarajiwa kukamuliwa mafuta kiasi cha lita zipatazo 34, 380," amesema Nyihita.
Amesema kuwa, changamoto zilizopo ni pamoja na upungufu wa fedha kuendeshea mradi,gharama kubwa za mbegu za alizeti, upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo na ukosefu wa umeme.
Vile vile,ameiomba Serikali kutoa rasilimali ardhi kwa wingi ili kupambana na upungufu wa mafuta ya kula hapa nchini.
Katika ziara yake mkoani Mara, Rais huyo wa TCCIA ametembelea pia kiwanda cha Nyihita Sunflower Cooking Oil Production kilichopo Nyanchabakenye Wilaya ya Rorya mkoani humo, kutembelea ofisi za kitega uchumi za TCCIA mkoa zilizopo Kata ya Bweri Manispaa ya Musoma.
Sambamba na kiwanda cha Credo Leather Products Rorya na pia amefanya mazungumzo na wafanyabiashara wa Mkoa wa Mara katika Ukumbi wa uwekezaji uliopo ofisi ya mkuu wa mkoa huo.