TFRA,wazalishaji wa mbolea waazimia utoshelevu wa mbolea nchini

DAR ES SALAAM-Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imekutana na kufanya mazungumzo na wazalishaji wa mbolea nchini ambapo wamejadili mustakabali wa tasnia ya mbolea wenye lengo la kupunguza uingizaji wa mbolea ifikapo mwaka 2030.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka, Joel Laurent wakati wa kikao baina ya TFRA na wazalishaji wa ndani wa mbolea kilichofanyika tarehe 20 Machi, 2024 katika ukumbi wa mamlaka jijini Dar Es Salaam.

Amesema, kupungua kwa utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchini kutapunguza matumizi ya fedha za kigeni na hivyo kuongeza mchango wa Sekta ya Kilimo kwenye Uchumi wa Taifa na kufikia asilimia 10.

Akizungumza mara baada ya kikao hicho, Mkurugenzi Laurent amesema, maono ya Mhe.Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ifikapo 2030 ni kuhakikisha nchi inajitegemea kwa asilimia 100 katika kupata pembejeo ya mbolea kwa kutumia viwanda vya ndani.

Ameeleza kuwa, ili kufikia azima hiyo, Mamlaka imekutana na wazalishaji wa ndani ili kujadiliana maeneo ya kufanyia kazi ili kuwawezesha kutatua changamoto wanazokabiliana nazo kutakakopelekea kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo na hivyo nchi kujitosheleza.
Laurent amebainisha kuwa, Ili kufikia ajenda 10/30: Kilimo ni Biashara, juhudi zinafanyika ili kuongeza kiasi cha mbolea inayotumika kwenye hekta 1 kutoka kg. 19 mpaka wastani wa kilo 50 kwa hekta moja.

Amesema, wastani wa mahitaji ya mbolea kwa mwaka ni takribni tani 848,000 kwa mbolea zote na kueleza kuwa matarajio ya mamlaka ni kuongezeka kwa matumizi ya mbolea ifikapo 2030 kutakakotokana na uelewa wa manufaa ya kutumia mbolea kwenye kilimo.

Pia, uzingatiaji wa kanuni bora za kilimo kama zinavyoelekezwa na Maafisa Ugani wetu katika maeneo yao, wakulima kuhamasishwa kutumia mbolea zinazozalishwa nchini pamoja na bei ya bidhaa hiyo kuwa himilivu kutakakopelekea kila mkulima kumudu gharama hizo.
Kwa upande wake, Tosky Hans ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Minjingu Mining and fertilizer, ameipongeza Mamlaka kwa kuitisha kikao kilichoangazia namna tasnia ya mbolea nchini inavyoweza kuongeza uzalishaji na utoshelevu kulingana na mahitaji ya nchi.

Amesema, huu ni mwanzo mzuri na kuishauri TFRA kuyaingiza yote waliyokubaliana kwenye matendo ili yasaidie nchi katika kufikia azma ya kujitosheleza kwa mahitaji ya mbolea nchini na nchi jirani.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Hapco Tanzania Limited, Conrad Massawe amesema, TFRA imekuwa ikishirikiana na wadau kwa muda mrefu na kuhakikisha mkulima anapata mbolea bora na kwa bei himilivu na kueleza kikao kilichofanyika kimekuwa na manufaa makubwa na kuomba moto ulioanzishwa na Mamlaka uendelee.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Mbolea Itracom Nduwimana Nazaire amempongeza Mkurugenzi Laurent kwa juhudi anazozifanya katika kutatua changamoto za wazalishaji wa mbolea nchini.

Amesema,kikao hicho ni mwendelezo wa yaliyojadiliwa wakati wa ziara ya kiongozi huyo kwenye viwanda vya mbolea nchini na Itracom ikiwepo.
Amesema mpaka sasa kiwanda chake kina uwezo wa kuzalisha tani laki 8 na wanatarajia mpaka mwezi Juni watakuwa wamekamilisha ujenzi utakaopelekea kuzalisha kiasi cha tani milioni 1 kwa mwaka na kubainisha wako katika hatua za mwsho wa ujenzi wa kiwanda hicho.
Akitaja maazimio ya kikao hicho, William Ngereja ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Itracom alisema ni pamoja na TFRA wakishirikiana na wazalishaji wa ndani wa mbolea kuja na sera, kanuni na sheria zitakazosaidia kulinda wazalishaji wa ndani wa mbolea.

Sambamba na namna bora ya kufikisha mbolea kwa wakulima, namna bora ya kuboresha unufaikaji wa ruzuku ya mbolea inayotolewa na serikali.

Pia, namna bora ya kuagiza mbolea zinazotoka nje kama malighafi kwa viwanda vya ndani na mwisho wamepanga kukutana baada ya siku chache zijazo ili kupata mrejesho wa maazimio waliyoyafikia katika kikao cha leo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news