TFS:Juhudi za Rais Dkt.Samia zimepaisha utalii wa ikolojia,mapato nchini

NA GODFREY NNKO

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeeleza kuwa, juhudi za makusudi zilizochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan za kutangaza vivutio vya utalii nchini zimeleta matokeo chanya kwa wakala huo kupitia utalii wa ikolojia.
Hayo yamesemwa leo Machi 19,2024 jijini Dar es Salaam na Kamishna Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS),Prof.Dos Santos Silayo katika kikao kazi na wahariri wakiwemo waandishi wa habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Wakala umefaidika kutokana na juhudi za makusudi zinazochululiwa na Serikali ikiwemo ubunifu wa Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wa kuandaa filamu ya The Tanzania Royal Tour ambayo imetangaza nchi yetu ndani na nje ya nchi."

Prof.Silayo amebainisha kuwa,juhudi hizo zimewezesha kuongezeka kwa watalii wanaotembelea vituo vya utalii ikolojia kutoka 59,606 mwaka 2020/21 hadi kufikia watalii 242,824 mwaka 2022/2023.

Amefafanua kuwa, mapato katika kipindi hicho yaliongezeka kutoka shilingi milioni 154.96 hadi kufikia shilingi bilioni 1.5.

"Haya ni mafanikio makubwa kuwahi kupatikana kwa wakala katika sekta ya utalii, eneo la utalii wa ikolojia kuliko wakati mwingine wowote."

Katika hatua nyingine, Prof.Silayo amesema, wakala umejiwekea malengo ya kufikia rekodi mpya kwa kufikia watalii 500,000 huku matarajio yakiwa ni kufikia makusanyo ya shilingi bilioni tatu ifikapo mwaka 2025.

TFS ambayo ipo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii huku ikiwa miongoni mwa taasisi na mashirika yaliyopo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ulianzishwa kisheria kupitia Tangazo la Gazeti la Serikali (GN 269) la Julai 30,2010 na kuzinduliwa rasmi Julai 18,2011

Kuanzishwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu ni kwa mujibu wa Sheria ya Wakala "The Executive Agencies Act Cap. 245 (Revised Edition 2009)”, pamoja na Sera ya Misitu ya mwaka 1998.

Nyingine ni Sera ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998, Sheria za Misitu na Nyuki Sura 323 na Sura 224 za mwaka 2002.

TFS iliundwa kwa kuzingatia Programu ya Serikali ya Maboresho katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2000 (Public Service Reforms Programme (PSRP 2000)).

Programu hii ililenga kuimarisha Idara na Wakala (Ministerial Departments & Agencies (MDAs)) katika kuhakikisha utoaji wa huduma bora na madhubuti katika utumishi wa umma, ambapo wakala zinakuwa na uwezo, motisha na mbinu za mabadiliko yenye kuleta ufanisi na tija kiutendaji.

Aidha,TFS imeundwa kwa madhumuni ya kuhakikisha uwepo wa usimamizi madhubuti na wenye ufanisi na tija wa rasilimali za misitu na nyuki.

Wakati huo huo, Prof.Silayo amebainisha kuwa, kwa sasa TFS inasimamia misitu 464 ya hifadhi inayojuisha mashamba ya miti 24 na misitu ya mazingira asilia 23.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news