Thamani ya taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina yafikia shilingi trilioni 76

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imesema, thamani ya uwekezaji katika taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) imeongezeka kutoka shilingi trilioni 70 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 76 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 8.6.
Hayo yamesemwa leo Machi 24, 2024 jijini Dar es Salaam na Msemaji Mkuu wa Serikali,Mobhare Matinyi wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarani.

Matinyi ametaja sababu ya ongezeko hilo kuwa, ni Serikali ya Awamu ya Sita kuongeza mitaji kwa kiasi cha shilingi trilioni 5.5 katika mashirika ya kimkakati kwa maslahi ya taifa.

Aidha, amesema kuwa ofisi pia imeongeza makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi kutoka shilingi bilioni 637.66 hadi trilioni 1.008 kwa mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 58.

“Serikali pia imeongeza umiliki wa hisa katika kampuni ya almasi ya Williamson Diamonds kutoka asilimia 25 hadi 37 huku ikisaini mikataba ya ubia wa asilimia 16 zisizohamishika katika kampuni za madini,” amesema Matinyi.

Kuhusu TR

Ofisi ya Msajili wa Hazina ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa ofisi inayojitegemea kimuundo.

Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) ofisi ilikabidhiwa majukumu ya shirika hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news