NA LWAGA MWAMBANDE
MACHI 5, mwaka huu huzuni na majonzi vimetawala katika Kisiwa cha Paza kilichopo Wilaya ya Kusini Pemba, Zanzibar.
Ni kutokana na vifo vya watoto nane huku 78 wakilazwa hospitalini kwa kula nyama ya Kasa.
Kasa ni kiumbe wa majini hususani maji chumvi ambapo mara nyingi huwa anafananishwa na kobe.
Ingawa kobe anaishi nchi kavu, viumbe hao wawili wana vitu kadhaa kibaiolojia vinavyofanana.
Licha ya kasa kuishi majini, hutaga mayai yake ardhini na ana tabia ya kuyafukia mayai yake kwa mchanga ufukweni.
Aidha,tofauti na alivyo kobe, kasa hawezi kuingia ndani ya jumba lake, hivyo kichwa na miguu yake hubaki nje ya gamba muda wote.
Dkt.Haji Bakari Haji ameeleza kuwa, awali baada ya kufikishwa hospitalini, wagonjwa hao hawakutoa taarifa ya kilichowasibu, hata hivyo baada ya vipimo kuchukuliwa kwa uchunguzi zaidi ilibainika kuwa walikula nyama ya Kasa.
Hii si mara ya kwanza kutokea kwa tukio la kifo linalohusisha vifo vitokanavyo na ulaji wa kasa.
Mwaka 2021, watu saba ikiwa ni pamoja na mtoto wa miaka mitatu, walifariki kisiwani Pemba baada ya kula nyama ya Kasa mwenye sumu.
Pia, Oktoba, mwaka 2022 watu watatu akiwemo mtoto wa mwezi mmoja, wakazi wa Kijiji cha Rushungi Wilaya ya Kilwa,mkoani Lindi walifariki dunia na wengine 74 kukimbizwa katika vituo vya afya baada ya kula samaki Kasa mwenye sumu
Aidha,licha ya kuwa kitoweo maarufu miongoni mwa wakazi wa visiwani Zanzibar na maeneo ya Pwani,Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anashauri kuwa, yafaa tuache kula Kasa. Endelea;
Pengine kuna makosa, yafanya tuadhirike,
Vinasikitisha visa, kwetu bora vitoweke,
Msiba wa kula kasa, poleni sana wafiwa.
2.Wala sio mara moja, taarifa waandike,
Kwamba watu si mmoja, wale na waathirike,
Hapa ninajenga hoja, atumike vinginevyo,
Msiba wa kula kasa, poleni sana wafiwa.
3.Janga hili kuepuka, la kwamba kasa alike,
Ukubwa atambulika, watu wengi wahusike,
Tuone wanaanguka, kwa kweli mwisho lifike,
Msiba wa kula kasa, poleni sana wafiwa.
4.Kumla kuendelea, basi kitu kifanyike,
Vile tunapendelea, nyama yake itumike,
Vipimo kupendelea, ni lazima itumike,
Msiba wa kula kasa, poleni sana wafiwa.
5.Watu nane fikiria, hivihivi watoweke,
Na wengine wagumia, sipitali watibike,
Bora kuliangalia, lisisikikesikike,
Msiba wa kula kasa, poleni sana wafiwa.
6.Nyama yake ya kupimwa, kisha ndipo itumike,
Kama hiyo inaumwa, kwao watu isilike,
Ili wasije kuumwa, nap engine watoweke,
Msiba wa kula kasa, poleni sana wafiwa.
7.Pole kwa wote wafiwa, kutoka kwetu zifike,
Uchungu twauelewa, kwamba ndugu atoweke,
Bora ikafikiriwa, kasa wala asitumike,
Msiba wa kula kasa, poleni sana wafiwa.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602