DAR ES SALAAM-Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hammad Masauni amesema kuwa, wamebaini kuwepo kwa uanzishwaji holela na utitiri wa nyumba za ibada katika maeneo mbalimbali nchini.
Ameyasema hayo Machi 26, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Usajili wa Jumuiya za Kiraia itakayofanyika nchi nzima.
“Tumebaini uanzishwaji holela wa nyumba za ibada katika maeno mbalimbali nchi jambo ambalo linaweza kuchangia kwa usumbufu hususan zilizo kwenye makazi ya watu,"amesema.
Amesema, baadhi ya jumuiya za dini hususan makanisa na misikiti yamebainika kujengwa katikati ya makazi ya watu na kusababisha kuwepo kwa mrundikano wa taasisi nyingi kwenye eneo dogo.
Vile vile, baadhi ya taasisi kutumia sauti za juu na hivyo kusababisha hadha na usumbufu katika jamii.
“Kutokana na hali hiyo sasa tunafanya usajili wa jumuiya za kiraia ili zile zinazoenda kinyume na sheria tutazifuta,”amesema Waziri Masauni.