DODOMA-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ikiongozwa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali tarehe 19,2024 imefanya ziara kwenye mradi wa ujenzi wa jengo la Tume ya Madini Makao Makuu jijijni Dodoma kwa ajili ya kuona maendeleo ya ujenzi wake.
Viongozi wengine waliokuwepo ni pamoja na Watendaji kutoka Wizara ya Madini, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, Wakurugenzi na Mameneja kutoka Tume ya Madini.
Mara baada ya kufanya ziara na kupata maelezo kutoka kwa mkandarasi, imemtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kazi kwa kiwango bora na kwa wakati ili watumishi wa Tume ya Madini waanze kutumia jengo hilo mara moja.
Wakati huo huo akizungumza kwenye eneo la mradi, Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa Wizara ya Madini itahakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali sambamba na kupongeza Kamati kwa kutembelea mradi ameongeza kuwa Wizara ya Madini itasimamia ujenzi wa mradi kwa karibu zaidi kwa kila hatua ili kuhakikisha mradi unakamilika ifikapo Aprili 24, 2024.
Awali akiwasilisha taarifa ya ujenzujenzjengo, Katibu Mtendaji wa Tume, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa hadi sasa ujenzi wa jengo umefikia asilimia 87.5 na kuongeza kuwa sehemu iliyobakia ya asilimia 12.5 inakusudiwa kukamilishwa ndani ya kipindi kilichobaki.
Mhandisi Samamba amesema kuwa, mradi huu utakapokamilika utawezesha watumishi wote wa Tume ya Madini Makao Makuu kuwa katika jengo moja hivyo kuimarisha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi na wadau wengine.