Ujifanye umekufa

NA LWAGA MWAMBANDE

KUPITIA blogu yake, Christian Bwaya amewahi kuandika makala ambayo ilihoji kwa nini ni rahisi kumsifia mtu akifa kuliko akiwa hai?.

Alieza kuwa, hatupendi kuwasifu wengine wala kusikia wakisifiwa na wengine, lakini ni wepesi sana kumsifia marehemu.

Na ni nadra kusikia tabia ya marehemu ikikosolewa. Hata waliokuwa hawamsifii akiwa hai, huomba fursa ya kuusemea vizuri wasifu wa mpendwa aliyetutoka.

Mtu fulani maarufu akifa, kwa mfano, watu ambao hata siku moja hawakuwahi kumsema marehemu enzi za uhai wake, ndio huanza kushindana kutundika picha zake zikiambatana na maneno ya ‘apumzike kwa amani’.

Swali, kwa nini ni vyepesi kumsifia marehemu asiyesikia kuliko kumsifia binadamu anayesikia?.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande kutokana na hali hiyo anasema, mapenzi ya msibani yameshamkifu. Endelea;

1.Bora ufanye mpango, ujifanye umekufa,
Tukuletee michango, umalizie ghorofa,
Ukilalia mgongo, utabaki na ulofa,
Bora ufanye mpango, ujifanye umekufa.

2.Mapenzi ya msibani, miye yameshanikifu,
Tutasema masikini, anasubiri jokofu,
Tutajadili njiani, na wema wako wasifu,
Bora ufanye mpango, ujifanye umekufa.

3.Ukifa tutawaona, wale wanataka sifa,
Watashughulika sana, kama kazi ya tarafa,
Waonekane kwa kina, wanakujali ukifa,
Bora ufanye mpango, ujifanye umekufa.

4.Hata wasokuwa ndugu, wakijua mtu kafa,
Hawabaki na usugu, wanasafiri masafa,
Wanauza hata njugu, waje kuzitoa ofa,
Bora ufanye mpango, ujifanye umekufa.

5.Hadithi tunasikia, za watu sio malofa,
Ndugu wasiosikia, walitunga maarifa,
Kwamba mtu kaishia, watu watoke masafa,
Bora ufanye mpango, ujifanye umekufa.

6.Walisikia ya kwamba, umebanwa na kifafa,
Na kwamba wewe waomba, dawa kutoka kwa Tofa,
Wakatuna kama simba, nyumbani kwenye masofa,
Bora ufanye mpango, ujifanye umekufa.

7.Kusikia umevuta, wengi watatuma ofa,
Badae waje kukuta, msibani wana sifa,
Wakikuta hujadata, watabaki wakisafa,
Bora ufanye mpango, ujifanye umekufa.

8.Siigize kama wale, niwaitao malofa,
Wabeza Injili ile, kujipatia misifa,
Ona waumini wale, jinsi walivyo mafafa,
Bora ufanye mpango, ujifanye umekufa.

9.Pale wakikuuliza, kwenye hilo lako sofa,
Anzia kuwaeleza, kwamba hauna kifafa,
Na wakome kupuuza, uzima kuliko kufa,
Bora ufanye mpango, ujifanye umekufa.

10.Wengine ukiwajuza, unakaribia kufa,
Kusevu hawataweza, waseme muongo Kefa,
Ndipo utajiuliza, maiti waipa sifa?
Bora ufanye mpango, ujifanye umekufa.

11.Njia ya kuua watu, ndio yetu maarifa,
Ruhusa hunyimwi katu, ukisema ndugu kafa,
Hata ukitaka kitu, wapewa bila marefa,
Bora ufanye mpango, ujifanye umekufa.

12.Hata hivyo sio vema, kutukuza mtu kufa,
Bora kuacha alama, kwa mgonjwa asokufa,
Hivyo usijekukoma, kufeki ameshakufa,
Bora ufanye mpango ujifanye umekufa.

13.Mungu tupe kupendana, kabla hatujakufa,
Na vitu tukipeana, vitucheleweshe kufa,
Itakuwa safi sana, hata badae tukifa,
Bora ufanye mpango, ujifanye umekufa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news