Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA) ilianzishwa Julai 1, 1996 kwa uamuzi uliofanywa na Wizara ya Maji kuanzisha Mamlaka za maji chini ya Bodi ya Ushauri katika hali ya kugharimia sehemu ya uendeshaji (semi-autonomous).
Uamuzi huo ulihalalishwa na sheria ya maji kwa wakati ule, sheria namba 8 ya mwaka 1997. Serikali iliipandisha MWAUWASA kuwa Daraja ‘A’ ili kujiendesha bila kupata ruzuku yoyote kutoka serikalini (full autonomous) kwa Waraka wa Serikali namba 61 wa tarehe 13/02/1998.
Aidha,MWAUWASA inamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.
Ikiongozwa na DHIMA na ADHIMA yake, MWAUWASA inatekeleza majukumu yake ya kutoa huduma ya majisafi na uondoshaji majitaka (usafi wa mazingira) jijini Mwanza katika wilaya za Nyamagana na Ilemela pamoja na eneo la Kisesa wilayani Magu.
Majukumu hayo yanatekelezwa kwa kuzingatia Sheria ya Majisafi na Usafi wa Mazingira namba 12 ya mwaka 2009; Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002,
Miongozo mbalimbali toka EWURA; Mkataba wa Utendaji (performance contract) kati ya Wizara ya Maji na MWAUWASA pamoja na miongozo mingine mbalimbali inayotolewa mara kwa mara na Wizara ya Maji.