RUVUMA-Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Songea Vijijini imeahidi kushughulikia na kuupatia ufumbuzi mgogoro wa ardhi katika Kitongoji cha Msiri na Hifadhi ya Maliasili kilichopo katika Kijiji cha Nakahengwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akimuombea kura na kumnadi Mgombea Udiwani kwa tiketi ya CCM,Optatus Ndau katika Mkutano wa Kampeni uliofanyika Kijiji cha Nakahegwa Kata ya Mbinga Mhalule.
Kauli hiyo ameitoa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Peramiho tarehe 15 Machi,2024 katika Kijiji cha Nakahengwa wakati akimnadi Mgombea Udiwani,Optatus Ndalu, ambapo uchaguzi mdogo unatarajiwa kufanyika tarehe 20 Machi, 2024 baada ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo ya Mbinga Mhaule kufariki.
Wananchi wa Nakahengwa wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho akizungumza katika mkutano wa kumnadi Mgombea Udiwani katika Kata ya Mbinga Mhalule kwa tiketi ya CCM.
Aliongeza kuwa, wamejipanga kuhakikisha migogoro yote ya ardhi katika Kijiji cha Nakahengwa inamalizika na watu wanaishi kwa amani.
Viongozi wa CCM wa Wilaya ya Songea Vijijini na wananchi wa Kijiji cha Nakahegwa wakiongozwa na vijana wa usafirishaji abiria kwa pikipiki (bodaboda) wakimlaki Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama (Mb) Peramiho kabla ya mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kijiji cha Nakahengwa.
"Tunahitaji kuona kila mgeni anayeingia katika Kijiji cha Nakahengwa, hafikirii kuondoka kwa sababu wenyeji wa hapa ni wakarimu na wenye upendo,"amesema.
Katika hatua nyingine Waziri Mhagama amewakumbusha wananchi umuhimu wa kuchagua mgombea wa udiwani atakayeendelea kuchochea miradi ya maendeleo na kusimamia vyema ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akiwa amembeba mtoto wakati akizungumza na akinamama wa Kijiji cha Nakahengwa kabla ya Mkutano wa Kampeni uliofanyika katika kijiji hicho.
Alikumbusha kuhusu uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2020, "tuliomba mchague Mafiga Matatu ya Chama Cha Mapinduzi ili tujipange sawa sawa katika kushughulikia matatizo ya wananchi."
"Serikali kupitia ilani ya Chama Cha Mapinduzi imeshaanza kushughulikia bei ya mbolea kwa kuhakikisha inaendelea kushuka ili kusaidia wananchi,"alibainisha.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) pamoja na Mgombea Udiwani kwa tiketi ya CCM,Optatus Ndau wakicheza Ngoma kabla ya Mkutano wa Kampeni uliofanyika katika Kijiji cha Nakahengwa kata ya Mbinga Mhalule.
Muunganiko wa mafiga haya matatu unaongozwa na Serikali ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umesaidia katika kupandisha bei ya mahindi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Vijijini,Thomas Masolwa amesema ujenzi wa miundombinu bora ya barabara, miundombinu ya afya, miundombinu ya elimu na nishati ya umeme inasimamiwa na ilani ya Chama Cha Mapinduzi.
Wananchi wa Nakahengwa wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akizungumza katika Mkutano wa kumnadi Mgombea Udiwani katika kata ya Mbinga Mhalule kwa tiketi ya CCM.
"Sasa tunatembea na ajenda ya kuziba pengo katika Kata ya Mbinga Mhalule kwa kutafuta mtu atakayendelea kusimamia na kuchochea miradi ya maendeleo kwa wananchi.
"Kumpigia kura mgombea wa Chama Cha Mapinduzi ni kupigia kura maendeleo yanayoendelea kutekelezwa na Serikali," alibainisha.
Wananchi wa Kijiji cha Nakahegwa wakiwa wamembeba kwa furaha mgombea wa udiwani katika Kata ya Mbinga Mhalule kwa tiketi ya CCM,Optatus Ndau Wakati wa Mkutano wa Kampeni.
Naye mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, Optatus Ndau ameahidi kuendelea kusimamia miradi yote inayotekelezwa katika Kata ya Mbinga Mhalule.
Sambamba na hilo,Ndau ameahidi kuendelea kusimamia migogoro yote ya ardhi ya mashamba na mipaka katika Kata ya Mbinga.