Wanawake siku yenu, tambua tunawapenda

NA LWAGA MWAMBANDE

LEO Machi 8, 2024 wanawake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameungana na wenzao duniani kote kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Siku hii ambayo inaongozwa na kauli mbiu ya "Wekeza kwa Wanawake, Ongeza kasi ya Maendeleo", hapa nchini tumeshuhudia wanawake kutoka taasisi, mashirika na idara mbalimbali wakishiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kugusa maisha ya wenye uhitaji.

Wanawake hao wamekuwa wakifanya hivyo, ni sehemu ya kuwabariki wengine ikizingatiwa kuwa, siku hii inatambua mafanikio ya wanawake, bila kujali utaifa, kabila, dini, utamaduni, lugha, hali ya kiuchumi au mwelekeo wa kisiasa.

Siku ya Wanawake Duniani ilitambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa mnamo 1977 baada ya kuibuka kwa mara ya kwanza kutoka katika shughuli za harakati za wafanyakazi mwanzoni mwa karne ya 20 huko Amerika Kaskazini na Ulaya.

Mwaka huo, Umoja wa Mataifa ulipitisha Azimio Na. 32/142, kutangaza Siku ya Haki za Wanawake na Amani ya Kimataifa kuadhimishwa kila siku ya mwaka. 

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasema,wakati wanawake wanasherehekea siku yao hii, pia wanapaswa kutambua kuwa, tunawapenda. Endelea;

1.Wanawake siku yenu, tambua tunawapenda,
Twatoka matumbo yenu, jueni tunawapanda,
Twanyonya matiti yenu, elewa tunawapenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda.

2.Twajengwa malezi yenu, msihofu twawapenda,
Na hata chakula chenu, twakipenda twawapenda,
Sasa leo siku yenu, endeleeni kupanda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda.

3.Mpate elimu yenu, mbele zidisheni kwenda,
Kulea watoto wenu, jua wote wawapenda,
Kuendesha mambo yenu, mjue tunawapenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda.

4.Hebu jifanyie yenu, yale moyo unapenda,
Kama ni miradi yenu, maisha yazidi panda,
Pateni mikopo yenu, twajua mnakokwenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda.

5.Yafanyeni mambo yenu, familia zitapanda,
Bila ubunifu wenu, jua kwamba tutapinda,
Huo ni wajibu wenu, hata bila ya kupenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda.

6.Kupitia kazi zenu, na taifa litapanda,
Uchakarichaji wenu, mjue tunaupenda,
Furahieni kivyenu, jua sote twawapenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda.

7.Mwapendeza sare zenu, mwapendeza twawapenda,
Ishike nafasi yenu, nasi mzidi tupenda,
Vile ni watoto wenu, kwa malezi mwatulinda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda.

8.Wengine waume zenu, kutuombea mwapenda,
Hata marafiki zenu, uwepo wetu mwapenda,
Nanyi kwa imani zenu, Mungu zidi kumpenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda.

9.Kuwapa nafasi yenu, na vile anawapenda,
Maisha ni chanzo chenu, vinginevyo tungepinda,
Twatamba uzazi wenu, dunia mnaipenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda.

10.Sasa hii siku yenu, tambua tunawapenda,
Ni yetu sherehe yenu, siku hii twaipenda,
Na hamko peke yenu, elewa tunawapenda,
Msalie na amani, mkijua twawapenda.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news