DAR ES SALAAM-Walimu wa shule za Sekondari Vetenari, Temeke, Sandali na wanafunzi wa Shule ya ya Temeke jijini Dar es Salaam wamepewa elimu ya mbolea na kuombwa kuwa mabalozi wema kwenye jamii zao juu ya matumizi sahihi ya mbolea.

Diwani wa Kata ya Sandali, Christopher Mwansasu (katikati), Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondali Temeke Ingia Mtenga(kushoto) na Afisa Udhibiti Ubora wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Gema Nganyagwa (kulia) wakiwa katika picha mafunzo ya matumizi sahihi ya mbolea katika viwanja vya shule ya sekondari Temeke yakiendelea tarehe 5 Machi, 2024 wanawake wakirithisha ujuzi kwa waalimu na wanafunzi.

Elimu hiyo imetolewa na wawakilishi wa watumishi wanawake wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ikiongozwa na Gema Nganyagwa Afisa Udhibiti Ubora ikiwa ni moja ya shughuli zinazotekelezwa kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 machi, 2024.
Akizungumza wakati wa tukio hilo Diwani wa Kata ya Sandali Mhe. Christopher Mwansasu ameeleza kuwa, Tfra ni taasisi ambayo inayotambua na kushirikiana na jamii inayoizunguka katika hali zote.
Ameeleza kuwa, wamekuwa wakishirikiana sana katika shughuli mbalimbali za maendeleo na ndio maana wameona ni vyema kufika na kutoa elimu ya mbolea kwa wanafunzi wa shule hiyo iliyopo katika jamii yao.

"TFRA wanatambua kuwa elimu inaanzia chini na ndio maana wamechagua kundi hili ili kupanda mbegu inayowaandaa na kuwaonesha fursa zilizopo kwenye tasnia ya mbolea" amesema Diwani Mwansasu.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Temeke, Ingia Mtenga, ameishukuru TFRA kwa kuichagua shule anayoisimamia na kutoa elimu iliyowaongezea uelimu wa tasnia ya mbolea wanafunzi na waalimu wao.
Amesema, shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 2767 miongoni mwao wanafunzi 501 ni wa kidato cha 5 na 6 huku ikiwa na jumla ya walimu 60 na walimu 28 wakiwa ni wanawake.
Katika kuonesha uelewa walioupata kupitia elimu iliyotolewa wanafunzi waliulizwa maswali ikiwa ni pamoja na kutaka kujua tofauti kati ya mbolea za viwandani na samadi na kuhoji ni mbolea ipi inafaa zaidi.


Pia, wanafunzi hao walipenda kujua namna Mamlaka inavyodhibiti mbolea zinazozalishwa nchini lakini pia zile zinazoingizwa kutoka nje ya nchi na kupewa majibu Mujarabu kwa maswali yote yaliyoulizwa kutoka kwa wanawake hao.