Wanawake Tume ya Madini walipia bili za wagonjwa wenye uhitaji Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma

*Wananchi wengi waguswa na tukio hilo na kupongeza Tume ya Madini

DODOMA-Ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani leo Machi 06, 2024 wanawake kutoka Tume ya Madini wamefanya ziara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kulipia gharama za matibabu kwa wagonjwa wenye uhitaji maalum ikiwemo vifaa tiba, dawa, operesheni pamoja na kugawa baadhi ya vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuwatia moyo wagonjwa hao.
Akizungumza kwa niaba ya wanawake wa Tume ya Madini, Meneja wa Utawala na Rasilimali Watu, Fatma Chondo amesema kuwa ziara hiyo ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika tarehe 08, Machi 2024 ambapo wameamua kuwatembelea wagonjwa wenye uhitaji, kuwapatia msaada na kuwatia moyo.

“Tunatambua kila mtu ana mahitaji mbalimbali lakini nashukuru kwa michango iliyotolewa na Tume ya Madini kufanikisha kulipia baadhi ya gharama kwa wagonjwa 13 ambao wamekuwa wakipatiwa matibabu lakini wamepata changamoto ya kulipia gharama za kutibiwa,” amesema Chondo.
Ameendelea kusema kuwa, “Natoa wito kwa wanawake wengine kuwa sisi kama walezi tunategemewa na tuendelee kuwasaidia watanzania wenzetu wenye mahitaji zaidi lakini wanakosa msaada, ambapo kutoa ni akiba ya baadae pamoja na familia zetu.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Tegemea Jassel ameshukuru wanawake wa Tume ya Madini kwa umoja huo na kusisitiza wanawake wengine kujitokeza ili kuondokana na matatizo yanayowakabili wagonjwa.
Naye Muuguzi Mfawidhi Msaidizi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Mariam Lyimo ameshukuru kwa jitihada zilizofanywa na wanawake na kusisitiza kuendelea kujitokeza katika kuwasaidia wenye mahitaji maalum na walioshindwa kupewa matibabu kama wanawake wa madini.
Mmoja kati ya wagonjwa walionufaika na msaada huo, Daudi Muna ameushukuru uongozi wa Tume ya Madini kwa jambo walilofanya la kuwapatia msaada na kuongeza kuwa imewatia moyo sana na kujiona wa thamani sana katika jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news