KAGERA-Masanja Igolola ambaye ni Afisa Manunuzi Chuo cha Ufundi Stadi (VETA), Ndorage pamoja na Denis Rwegalulila mzabuni wamelipa faini ya shilingi milioni moja na kurejesha shilingi milioni 2.8 walizojipatia kwa manunuzi hewa.
Uamuzi huo umefikiwa Machi 15, 2024 katika Mahakama ya Wilaya Muleba mkoani Kagera mbele ya Mheshimiwa Hakimu Lilian Mwambeleko.
Kesi hiyo ya Jinai namba 3/2024 ilikuwa ya Jamhuri dhidi ya Bw. Masanja Igolola ambaye ni Afisa Manunuzi Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) , Ndorage pamoja na Denis Rwegalulila mzabuni.
Walishtakiwa kwa kosa la hongo katika manunuzi ambapo wanadaiwa kufanya manunuzi hewa mwaka 2019 ya mashine aina ya Porker Vibrator High F,hivyo kujipatia manufaa yasiyo stahiki ya shilingi milioni 2.8.
Kupitia kesi hiyo ambayo iliendeshwa na Wakili Kelvin Murusuri, Mahakama iliwakuta na hatia na kuwaamuru walipe faini ya shilingi milioni moja au kutumikia kifungo cha miaka miwili jela.
Vilevile, Mahakama iliwataka warejeshe fedha hizo zote shilingi milioni 2.8 walizojipatia kwa manunuzi hewa.
Aidha, washtakiwa wamelipa faini ya shilingi milioni moja na kurejesha shilingi milioni 2.8 katika ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Muleba.
Mbali na hayo,Shauri la Rushwa Na. O4$/2024 limetolewa uamuzi.
Kesi hii ni ya Jamhuri dhidi ya Bw. Raysone Baliyeguje ambaye ni mkusanyaji wa mapato kwa njia ya POS katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.
Mtuhumiwa alishitakiwa kwa kosa la hongo kinyume na Kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329/2022.
Ni kwa kujipatia manufaa yasiyostahili wakati wa ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali shilingi 5,292,900 hivyo kufanya upotevu wa shilingi 5,292,900 mali ya Halmashauri ya Muleba.
Kesi iliongozwa na Wakili Kelvin Murusuri ambapo Mahakama imemhukumu mshitakiwa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 500,000 au kwenda jela miaka miwili na kurejesha fedha zote ndani ya miezi mitatu.
Hata hivyo mshtakiwa amerejeshwa gerezani akisubiria taratibu za kulipa faini hiyo.