Wazee waliopigana Vita vya Pili vya Dunia wakutana Dar, Serikali yatoa wito

DAR ES SALAAM-Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, Sixtus Mapunda amefungua Mkutano Mkuu wa nane wa Chama cha Wastaafu waliopigana Vita ya Pili ya Dunia (TLC) huku akisisitiza wazee hao kushirikiana na serikali ili kuendelea kutunza historia hiyo.
Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanyika leo jijini Dar es salaam,Mapunda amesema chama hicho ni muhimu katika kutunza historia ambayo vijana wengi hawaifahamu.

"Ni vyema Sasa ushirikiano ukawepo kati ya wazee hao na wakuu wa Mikoa na Wilaya kwenye matawi yao ili kukiimarisha na kutunza historia kwa faida ya kizazi kijacho."

Amesema, wazee 52 walio hai hadi sasa kati ya Wazee 15,000 walioshiriki vita ya pili ya Dunia ni hazina kwa taifa na wenye historia na nchi na kwamba wao ndio waliosababisha Tanzania kuwa kisiwa Cha amani na utulivu.

“Tumeambiwa kuwa kwenye vita ya pili ya Dunia mwaka 1939 hadi 1945 ambavyo sisi wote hapa tulikuwa hatujazaliwa,watu takribani 15,000 walishiriki na waliorudi ni takribani 13,000 na hadi sasa waliohai ni 52 na mdogo zaidi ana miaka 100 hivyo ni muhimu kuwaandikia historia kabla hawajafa au kupoteza kumbukumbu,"amesema Mapunda.Hata hivyo, ametoa wito kwa waandishi wa habari kuwatafuta wazee hao waliopigana Vita ya pili ya Dunia na kutengeneza makala ambazo zitawezesha kuweka historia nzuri hususani na picha ambazo zitawasaidia vijana na kizazi kijacho kujua historia ya nchi yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TLC, Hamis Kwizombe amesema kuwa wazee hao wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutotambuliwa na serikali.

Aidha,ameiomba serikali kuwasimamia katika kutunza Wazee hao kwani ndio waliobakia na ni tunu ya taifa ambayo imewakutanisha na inayofanya watu wengi kukimbilia Tanzania kama kisiwa cha amani waliyoipigania Wazee hao.

Naye Katibu Mkuu wa Chama hicho Charles Lubara ametoa rai Kwa wanachama hao kushirikiana na kuwa pamoja Kwa lengo la kuhifadhi historia ya Wazee kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho.

Amesema, tayari wamewasiliana na Wizara ya Maliasili ambapo wamepewa eneo Dodoma ambalo watajenga makumbusho itakayotumiwa na watu mbalimbali kwenda kujifunza historia ya nchi yao.

Katika mkutano huo pia wamewachagua Kwa mara nyingine viongozi watakao kiongoza chama kwa miaka mitatu ijayo.

Viongozi hao ni Hamis Kwizombe ambaye anaendelea na nafasi yake ya uenyekiti, Charles Lubara anaendelea na nafasi yake ya ukatibu Mkuu, Kapteni Mohamed Ligora anaendelea na nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini na Chief William Machimu amechaguliwa kuwa Katibu wa Bodi ya Wadhamini.

Aidha,Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Kapteni Mohamed Ligora amesisitiza uzalendo wa kulithishwa historia hiyo Kwa vizazi vijavyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news