ARUSHA-Waziri wa Madini,Mhe. Anthony Mavunde ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa, wizara itaufanyia kazi ushauri uliotolewa wa kuhakikisha mradi wa jengo la ghorofa nane la Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) linakidhi mahitaji ya watumiaji kwa kipindi kirefu.
Ameyabainisha hayo leo Machi 13, 2024 wakati wa ziara ya kamati hiyo ilipotembelea eneo linapotarajiwa kujengwa jengo la ghorofa nane la TGC katika Kata ya Themi-Njiro jijini Arusha.
Ikiwa ni sehemu ya utanuzi wa miundombinu ya kituo hicho kilicho chini ya Wizara ya Madini kinachojihusisha na utoaji mafunzo ya uongezaji thamani madini yakihusisha ukataji na ungarishaji wa madini ya vito.
Pia, utambuzi wa madini ya vito na utengenezaji wa bidhaa za usonara kama pete, hereni, mikufu, zikiwemo huduma mbalimbali kama maabara ya madini ya vito.
‘’Tutazingatia ushauri mzuri uliotolewa na Kamati ili ujenzi wa jengo hilo utakapo kamilika uwe wa kiwango cha kimataifa na kukidhi mahitaji ya watumiaji kwa kipindi kirefu ikizingatiwa kuwa eneo litakapojengwa jengo hilo ni nyeti, lipo karibu na mjini na rahisi kufikika,’’amesema Waziri Mavunde.
Waziri Mavunde amezitaja huduma zitakazokuwa ndani ya jengo hilo na kusema kuwa ni pamoja Ofisi za TGC, Ofisi za Madini kwa Mkoa wa Arusha, Viwanda vya uongezaji thamani madini vya wafanyabiashara, sehemu maalum ya kuendesha minada ya madini, maktaba pamoja na mabweni ya wanafunzi watakaojiunga na kituo hicho.
Amezitaja, huduma nyingine kuwa ni pamoja na maabara za Madini ya Vito na bidhaa za usonara, makumbusho ya Madini ya Vito na bidhaa za sonara na maduka ya bidhaa za Madini.

