DAR ES SALAAM-Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde amesema kuwa, Sekta ya Madini katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imepiga hatua kubwa.
Mavunde ameyasema hayo leo Machi 14, 2024 katika Kipindi cha Good Morning cha Wasafi TV ya jijini Dar es Salaam.
Amesema,Serikali katika kipindi cha kuanzia Machi 2021 hadi Februari 2024, wizara kupitia Tume ya Madini imeendelea kutekeleza jukumu la ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali yatokanayo na ada za mwaka za leseni.
Pia, ada za ukaguzi, ada za kijiolojia, mrabaha, fines, penalties and forfeitures na malipo ya huduma za maabara.
Mheshimiwa Mavunde amesema, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuanzia Machi, 2021 hadi Februari, 2024 jumla ya shilingi Trilioni 1.9 zilikusanywa kutokana na vyanzo hivyo.
Vile vile amesema, mchango wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka hadi kufikia asilimia 9.1 mwaka 2022.
Aidha,katika kipindi cha muda mfupi wa kati cha robo ya tatu (Julai-Septemba) ya mwaka 2023 sekta ilichangia asilimia 10.4 ikilinganishwa na mchango wa asilimia 9.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.
Waziri amesema, mwenendo huu wa mchango unaakisi dhamira ya Serikali kuhakikisha sekta hii inaimarika na kuweza kuchangia hadi asilimia 10 katika Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025.
Amesema, katika kipindi cha mwezi Machi, 2021 hadi Februari, 2024, wizara kupitia Tume ya Madini imeendelea kusimamia biashara ya madini katika masoko ya madini hapa nchini ili kuhakikisha yanafanya kazi kwa ufanisi.
Pia, amesema katika kipindi rejewa shughuli za uchimbaji na biashara ya madini zimeendelea kuongezeka ambapo jumla ya masoko 42 na vituo vya ununuzi wa madini 100 vimeanzishwa nchini.
Mbali na hayo, Mheshimiwa Mavunde amesema, katika kipindi cha mwezi Machi, 2021 hadi Februari, 2024 kiasi cha tani 52.9 za madini ya dhahabu, tani 1,204.83 za madini ya bati, karati 54,025.89 za madini ya Almasi,
Zikiwemo karati 183,551.87 na tani 121.34 za madini ya Tanzanite na kiasi cha karati 171,286.92 na tani 94,647.94 za madini mengine ya vito yaliuzwa katika masoko ya madini.
Amesema, mauzo ya madini hayo yamechangia makusanyo kwa maana ya mrabaha na ada ya ukaguzi kiasi cha shilingi bilioni 476.78.
Mhehimiwa Waziri Mavunde amesema, kwa kipindi cha miaka mitatu leseni za uchimbaji mkubwa wa madini mkakati zimetolewa, ambapo leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini adimu (rare earth elements) imetolewa kwa Kampuni ya Mamba Minerals Corporation Limited (MMCL).
Ni katika eneo la Ngualla lilipo Mkoa wa Songwe na leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini ya kinywe imetolewa kwa kampuni ya Faru Graphite Corporation Limited (FGCL) katika eneo la Mahenge lililopo Mkoa wa Morogoro.
Pia, amesema leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini ya heavy mineral sands kwa Kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited (NYSL) katika eneo la Tajiri, Wilaya ya Pangani,Mkoa wa Tanga inatarajiwa kutolewa wakati mfupi ujao.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Mavunde amesema, Serikali imeliwezesha Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kununua mitambo mitano (5) ya uchorongaji (Rig) kwa ajili ya kuwahudumia wachimbaji wadogo.
Amesema, mitambo hiyo imesambazwa katika maeneo ya Itumbi (Chunya), Lwamgasa (Geita), Katente (Bukombe), Buhemba (Butiama) na Dodoma.Ifikapo Juni 2024 mitambo yote itafikia idadi ya 15.
Vile vile, idadi ya Watanzania walioajiriwa kwenye migodi, Mheshimiwa Mavunde amesema imeongezeka kutoka 14,308 kati ya waajiriwa wote 14,742 sawa na asilimia 97 kwa mwaka 2021 hadi kufikia ajira 18,580 kati ya 19,165 sawa asilimia 97 hadi kufikia Februari 2024.
Aidha, idadi ya Watanzania wanaotoa huduma na kuuza bidhaa kwa wamiliki wa leseni za madini nchini, kwa mwaka 2023 jumla ya dola za Marekani Bilioni 1.65 zilitumika kununua bidhaa na huduma kwa kampuni za madini nchini.
Mheshimiwa Waziri amesema, manunuzi ya huduma na bidhaa kwa kampuni za Kitanzania yameongezeka kutoka dola za Marekani Milioni 713 ambayo ni sawa na asilimia 82 ya manunuzi yaliyogharimu kiasi cha dola za Marekani Milioni 874 kwa mwaka 2021 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 1.43.
Amesema, ongezeko hilo ni sawa na asilimia 86 ya kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.65 ya manunuzi yote yaliyofanyika mwaka 2023.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri amesema, wanajenga jengo la ghorofa nane la Kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) jijini Arusha kwa ajili ya shughuli za kituo hicho.
Jengo hilo litakuwa na miundombinu ya madarasa, mabweni ya wanafunzi, karakana za uongezaji thamani madini, maabara za madini ya vito, duka la bidhaa za usonara, ofisi na kantini.
Amesema,lengo ni kujiimarisha katika masuala ya uongezaji thamani madini ya vito na kufanya nchi yetu kuwa kitovu cha shughuli za madini ya vito katika Bara la Afrika.
Waziri Mavunde amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kufanya utafiti wa kina wa kijiolojia kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kurusha ndege “High Resolution Airborne Geophysical Survey” ili kuboresha taarifa za kijiolojia zilizopo katika vitalu sita vilivyoko katika maeneo mbalimbali ya nchi.