Waziri Mkuu ataka uwekezaji ATCL uwe kichocheo cha ukuaji wa uchumi

DAR ES SALAAM-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Uchukuzi kusimamia ipasavyo Shirika la Ndege Tanzania ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa unaleta matokeo chanya na kuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta nyingine mtambuka na uchumi kwa ujumla wake.
Amesema kuwa, ongezeko la ndege na huduma za usafiri inasaidia kuongeza fursa za biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.

Amesema hayo leo Jumanne, Machi 26, 2024 alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 737-9 Max, kwenye uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ili kuendelea kuikuza sekta ya anga nchini, Wizara ya Uchukuzi iandae mpango wa kuongeza wataalamu wazalendo katika fani zinazohusu masuala ya ndege hususan katika eneo la matengenezo na urubani.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa Shirika la Ndege Tanzania kuongeza uzalendo na kuwafichua wale wote wenye nia ya kulihujumu shirika hilo pamoja na kudhibiti upotevu wa mapato kupitia tiketi na mizigo.
Pia, amewataka viongozi na watendaji wa Shirika hilo wahakikishe ndege zote zinaendeshwa kwa tija kwa kufanya tafiti za kutosha wa masoko kabla ya kupeleka ndege.

Amesema kuwa, usafiri wa anga umekuwa chachu ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na biashara.
“Uwepo wa usafiri wa ndege umeongeza tija kubwa kwa wakulima hususan wa mazao ya mbogamboga na matunda, wafugaji na wafanyabiashara wa Kitanzania.”

Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya sita imesaini mikataba ya miradi mipya 6 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 674.3 inayohusu ujenzi wa kiwanda cha kujengea meli (shipyard) katika Ziwa Tanganyika, ujenzi wa meli kubwa ya kubeba mizigo tani 3,500 na meli nyingine yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mizigo ambayo inajengwa katika Ziwa Victoria.Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa sambamba na ununuaji wa ndege za abiria na moja ya mizigo, Serikali imenunua ndege mbili za mafunzo kwa ajili ya Chuo cha Usafirishaji (NIT) ili kusaidia kuongeza idadi ya marubani kwenye soko la ajira na kupunguza uhaba wa marubani nchini.

“Pia NIT imewezesshwa mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kutoa mafunzo ya shahada na Stashahada ya uhandisi wa ndege ili kuzalisha wahandisi na mafundi mchundo watakaoingia kwenye soko la ajira.”Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL),Mhandisi Ladislaus Matindi amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuijengea kampuni hiyo uwezo wa kutoa huduma kwa kuinunulia ndege mpya na kuijengea miundombinu wezeshi katika biashara ya anga.

“Hadi sasa Serikali imewekeza shilingi trilioni 2.4 katika ununuzi wa ndege, ujenzi wa mindombinu wezeshi ya kibiashara pamoja na ulipaji wa sehemu ya madeni yaliyolimbikizwa.”

Ameongeza kuwa,ATCL inaendelea kutekeleza mpango mkakati wake wa pili wa miaka mitano ulioanza mwaka wa fedha 2022/23 na kumalizia 2026/27 ambao pia unahusisha mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano yaani 2021/22-2025/26 ambao unatarajiwa kuiwezesha ATCL kuwa na ndege 20.“Hadi sasa ATCL ina ndege 14 zilizonunuliwa katika kipindi cha ufufuaji."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news