NA LWAGA MWAMBANDE
NI wazi kuwa, kwa hali ya kawaida kutoa ni moyo, kwani unaweza kuwa na vitu vingi, lakini ukawa mchoyo.
Vile vile, unaweza kuwa na vitu vichache,lakini ukawa mtoaji kwa watu au makundi mbalimbali.
Mara, nyingi yafaa kutambua kuwa, kama umesimama na Mungu vizuri na una uhakika upo katika njia sahihi, nyoofu ukiguswa kutoa, fanya hivyo bila kusita.
Lakini yakupasa kutambua kuwa, unapotenda wema usizidi uwezo, kwani ukizidi uwezo ni shida. Ungana na mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande kufahamu zaidi. Endelea;
1.Kwa ulivyobarikiwa, ndugu wengi watakuja,
Kina Salome na Musa, watajibeba pamoja,
Watakuja kwako kisa, eti wana shida moja,
Kama wewe una pesa, wema sizidi uwezo.
2.Wajao wengi ni sumu, wakung’ong’a wakitoka
Utadhani ni nidhamu, kumbe mali wakupoka,
Nia yao wajikimu, huku wewe wafutika,
Kama wewe una pesa, wema sizidi uwezo.
3.Siku utapofulia, jiji utalitambua,
Ndugu watavyokujia, wapate kukuumbua,
Hawatakufagilia, kwa mali wazochukua,
Kama wewe una pesa, wema sizidi uwezo.
4.Kufulia kuko kwingi, kwa afya hata na mali,
Ukiwa na vitu vingi, ugonjwa kwao halali,
Wao watakunywa tungi, wewe kitandani chali,
Kama wewe una pesa, wema sizidi uwezo.
5.Wakizipata fununu, wewe wataka ishia,
Watakitafuta kinu, mali yako kupigia,
Ukifa kifo cha KANU, wabaki washangilia,
Kama wewe una pesa, wema sizidi uwezo.
6.Nakuonya yote haya, ili uwe mwangalifu,
Usijedhani Wahaya, wote ni watakatifu,
Au watu toka Mbeya, moyoni wanakusifu,
Kama wewe una pesa, wema sizidi uwezo.
7.Ndo mana muda mwingine, onekana roho mbaya,
Wafikirie vingine, na kukuona mbaya,
Utokee kivingine, wenyewe waone haya,
Kama wewe una pesa, wema sizidi uwezo.
8.Wengi wetu twajifunza, wakati tumechelewa,
Wema mwingi watuponza, upepo tunatolewa,
Kujuta ndio twaanza, wakati tushanyolewa,
Kama wewe una pesa, wema sizidi uwezo.
9.Ndugu wengine si ndugu, wabaya kuliko fira,
Wasababisha vurugu, bila ya kujali sura,
Wang’oe kama magugu, watayaleta madhara,
Kama wewe una pesa, wema sizidi uwezo.
10.Chochote unachofanya, akuongoze Muumba,
Wema usijeufinya, muhitaji akiomba,
Mungu wewe kakufanya, usiringe na kutamba,
Kama wewe una pesa, wema sizidi uwezo.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602