VICTORIA FALLS-Waziri wa Madini wa Jamhuri ya Zimbabwe,Mhe. Soda Zhemu amesema kuwa, nchi yake imevutiwa na Mifumo ya Minada ya Madini ya Vito iliyo katika hatua za mwisho kurejeshwa nchini Tanzania baada ya kukamilika kwa Marekebisho ya Sheria.
Alisema hayo Machi 12, 2024 mjini Victoria Falls, nchini Zimbabwe katika kikao kifupi na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo anayeongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tisa wa Wataalam na Baraza la Mawaziri wa ADPA unaoendelea mjini hapa.

Aidha, Mbibo aliongeza kuwa, uwepo wa minada ya ndani ya nchi inatoa fursa kwa wenyeji kushiriki katika soko la madini ya vito kwa kuongeza thamani pamoja na kununua kwa matumizi yao pamoja na biashara.
Kufuatia maelezo hayo ya Mbibo, Waziri wa Madini wa Jamhuri ya Zimbabwe, Mhe. Soda Zhemu alikiri kuvutiwa na muundo wa minada ya madini ya vito iliyo kwenye hatua za mwisho kurejeshwa mara baada ya kukamilika Marekebisho ya Sheria kwa kusema kuwa ni wazo Nchi hiyo italichukua na kulifanyia kazi.
Ameeleza kuwa muundo wa minada iliyopo Zimbabwe haitoi nafasi kwa wenyeji kushiriki bali wageni wamekuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuongeza thamani na kununua madini hayo ya vito.

Kikao hicho kifupi, pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini – Zimbabwe, Pfungwa Kunaka, pamoja na Kamishna Msaidizi wa Madini – Sehemu ya Uendelezaji Uchimbaji Mdogo na Mratibu wa ADPA Tanzania, Francis Mihayo.