NA GODFREY NNKO
GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema,akiba ya fedha za kigeni nchini ni zaidi ya dola bilioni 5.3 mwishoni mwa mwezi Machi 2024, sawa na miezi 4.4 ya uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi.
"Ikiwa ni kiwango ambacho kipo juu ya lengo la miezi minne kama tulivyojiwekea kwa nchi yetu;
Ameyasema hayo leo Aprili 4,2024 katika ofisi ndogo za makao makuu ya Benki Kuu jijini Dar es Salaam mbele ya wakuu wa taasisi za fedha na vyombo vya habari.
Ni wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ambayo imetangaza ongezeko la Kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kutoka asilimia 5.5 hadi asilimia 6.
Uamuzi huo umefikiwa wakati wa kikao cha MPC kilichofanyika Aprili 3, 2024 kwa kuzingatia tathmini ya mwelekeo wa uchumi iliyofanyika mwezi Machi,mwaka huu.
Gavana Tutuba amesema, thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani ilipungua kwa asilimia 1.8 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 ikilinganishwa na asilimia 1.6 katika robo ya mwisho ya mwaka 2023.
"Hali hii ilitokana na msimu wa mapato madogo ya fedha za kigeni pamoja na mazingira ya kiuchumi duniani.
"Lakini, tunatarajia kutokana na mwenendo wa ukuaji uchumi hali hii itaendelea kuwa himilivu, kutokana na siku zijazo kuendelea kupatikana kwa dola nyingi zaidi kutokana na shughuli na mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Serikali,"amefafanua Gavana Tutuba.
Pia amesema, Benki Kuu itaendelea kusimamia uhimilivu wa shilingi na kuwezesha upatikanaji wa fedha za kigeni katika uchumi wa Tanzania.