MAPUTO-Katika jitihada za kuimarisha matumizi ya Lugha ya Kiswahili, tarehe 02 Aprili 2024, Mhe. Phaustine Kasike, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji ametembelea Shule ya Kimataifa ya Maputo (Maputo International School - MIS) iliyopo jijini Maputo.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 3,2024 na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Maputo,Msumbiji.
Ni kwa ajili ya kukagua Darasa la Kiswahili lililoanzishwa shuleni hapo kwa ushirikiano kati ya shule hiyo na Ubalozi wa Tanzania uliopo Maputo na pia kutathmini uendeshwaji wake.
Mkuu wa Shule hiyo, Prof. Lucas Mkuti aliushukuru Ubalozi wa Tanzania, Maputo kwa mchango mkubwa uliotoa katika kuanzishwa na kuendelezwa Darasa hilo.
Kwa upande mwingine, alieleza mikakati ya baadae ya Shule hiyo katika kuendeleza Lugha ya Kiswahili ikiwemo kufungua madarasa ya ziada kwa ajili wananchi wa kawaida tofauti na ilivyo sasa ambapo masomo hutolewa kwa wanafunzi wa Shule hiyo pekee.
Mikakati mingine ni kufungua Madarasa ya Kiswahili kwa njia ya mtandao (e-learning) pamoja na kuimarisha uhusiano na ushirikiano pamoja na Vyuo na Taasisi zinazohusika na Lugha ya Kiswahili nchini Tanzania.
Kwa upande wake, Mhe Balozi Kasike aliupongeza Uongozi wa MIS kwa mabadiliko makubwa waliyofanya Shuleni hapo ikiwemo kufungua madarasa ya Lugha za Kigeni na kuahidi kwamba Ubalozi utaendelea kutoa kila aina ya msaada na ushirikiano ili kuhakikisha Shule hiyo inatimiza malengo yake hususan yanayohusiana na ufundishaji wa lugha ya Kiswahili.