Benki ya TCB kuadhimisha miaka 100 mwakani

NA GODFREY NNKO

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) mwakani inatarajiwa kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake nchini.
TCB ni zao la Tanganyika Postal Office Savings Bank (TPOSB) ambayo ilianzishwa mwaka 1925 wakati ambapo Tanganyika ilikuwa chini ya utawala wa Uingereza.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara (TCB),Adam Charles Mihayo ameyasema hayo leo Aprili 9,2024 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).

Amesema, TCB imepitia katika hatua mbalimbali ambapo baadaye ilikuwa Benki ya Akiba chini ya lililokuwa Shirika la Posta na Simu la Afrika ya Mashariki (EAP&TC) na ilikoma kufanya kazi baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aidha, Shirika la Posta na Simu Tanzania (TP&TC) lilianzishwa ili kuhudumia soko la Tanzania.

Afisa, Mtendaji Mkuu huyo amesema, TPB iliundwa kutoka kwa TP&TC ambapo ilianzishwa kwa Sheria ya Benki ya Posta Tanzania Na. 11 ya mwaka 1991.

Juni 29, 2015, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liliifuta sheria hiyo na Machi 29, 2016 benki hiyo iliunganishwa chini ya Sheria ya Makampuni ( Sura ya 212) kama TPB Bank PLC.

Januari 19, 2017, benki ilizindua jina la TPB Bank PLC kwa umma pamoja na nembo yake mpya na Julai 14, 2021 benki ilibadilisha jina na kuwa Tanzania Commercial Bank Plc.

TCB inamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hisa asilimia 83.44, Shirika la Posta hisa asilimia 7.61, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hisa asilimia 2.91.

Wengine ni Posta na Simu Savings and Credit Cooperative Society Limited hisa asilimia 2.67,Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF hisa asilimia 2.35 na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) hisa asilimia 1.02.
Afisa Habari Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho amesema, lengo la vikao hivyo ni kuondoa ukuta au pazia ambalo wengi walihisi taasisi hizo za umma zimejifungia ndani na zinafanya mambo yake kimya kimya.

"Na hata changamoto zinapotokea na ikatolea umma umepewa hizo taarifa mapokeo yake ni tofauti," amesema Sabato huku akifafanua kuwa,

Baada ya vikao kazi hivi ambavyo vimewapa Watanzania mwanga wa kile kinachoendelea ndani ya taasisi na mashirika ya umma, wamekuwa na uelewa mpana na hata taarifa zinapotoka wanakuwa hawana maswali mengi.

"Kwa hiyo tunaamini kwamba, kitendo cha kufanya hii mikutano inakutanisha umma pamoja na hizi taasisi tukiamini kwamba jukwaa hili au kundi hili la wanahabari lina nguvu ya kufikisha ujumbe kuhusu hizi taasisi."

Katika hatua nyingine, Ofisi ya Msajili wa Hazina imewapongeza wanahabari kwa kuendelea kuwa na mchango chanya katika kufikisha elimu kwa umma kuhusu yale yanayofanywa na taasisi na mashirika mbalimbali ya umma nchini.

Amesema, vikao hivyo vinatoa fursa kwa taasisi na mashirika ya umma kueleza yalipotoka, yalipo, yanapoelekea na mafanikio yake kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news