NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza ukomo wa riba ya asilimia 6 katika robo ya pili ya mwaka 2024 kati yake na benki za biashara nchini.
Riba hiyo mpya itatumika katika kipindi cha robo ya pili kuanzia leo Aprili 4,2024 hadi Juni, mwaka huu.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, kwa niaba ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ametangaza riba hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Utekelezaji wa Sera ya Fedha kwa kutumia Mfumo wa Riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate) ulianza Ijumaa ya Januari 19, 2024 ambapo BoT iliachana na mfumo uliokuwepo wa Ujazi wa Fedha.
Katika robo ya kwanza ukomo wa riba ulikuwa asilimia 5.5 kati ya BoT na benki za biashara ili kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
"Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) imepandisha Riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate-CBR) kutoka asilimia 5.5 iliyotumika katika robo ya kwanza ya mwaka 2024 hadi asilimia 6, ambayo itatumika katika robo ya pili ya mwaka 2024, yaani mwezi Aprili hadi Juni 2024.
"Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika tarehe 3 Aprili 2024 na umezingatia tathmini ya mwelekeo wa uchumi iiliyofanyika mwezi Machi 2024."
Gavana Tutuba amesema,kamati imeona umuhimu wa kuongeza Riba ya Benki Kuu hadi asilimia 6, itakayokuwa na wigo wa asilimia 2 juu na chini, ili kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei siku zijazo kutokana na athari za mwenendo wa uchumi wa dunia.
Amesema,kutokana na tathmini ya mwenendo wa uchumi wa Dunia, kamati imebaini kuwa, katika robo ya kwanza ya mwaka 2024, ukuaji wa uchumi uliimarika katika nchi zilizoendelea na zile zinazoibukia kiuchumi.
"Mfumuko wa bei umeendelea kupungua, sambamba na kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha. Bei za bidhaa katika soko la dunia imebaki tulivu."
Benki Kuu ya Tanzania ni benki inayohudumia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar.
Pia ni benki ya taasisi za umma na benki za biashara. Kazi hizi ni kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006.