DODOMA-Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeidhinisha matumizi ya shilingi trilioni 10.125 kwa ajili ya Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), sekretarieti za mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa na taasisi zake kwa mwaka 2024/25.
Aidha,kati ya hizo fedha shilingi trilioni 3.415 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Fedha hizo zilizoidhinishiwa na Bunge zimeongezeka kwa takribani shilingi bilioni 900 ikilinganishwa na bajeti ya shilingi triloni 9.18 zilizoidhinishwa mwaka 2023/24.
Pia, Bunge limeidhinishia Ofisi ya Rais - TAMISEMI, taasisi zilizo chini yake, mikoa 26 ikijumuisha halmashauri 184 kukusanya maduhuli na mapato ya ndani ya shilingi trilioni 1.60.
Aidha, katika fedha zilizoidhinishwa shilingi bilioni 17.79 zinaelekezwa kwa ajili ya kuratibu na kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024.
Vile vile shilingi trilioni 1.02 zitatumika katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini.