MWANZA-Zaidi ya shilingi bilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka makusanyo ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.
Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Mheshimiwa Dkt. Angeline Mabula ameyasema hayo wakati akizungumza na kikundi cha Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) tawi la Kigala, Buswelu katika ukumbi wa ofisi za CCM Kata ya Kirumba.
Hiyo ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kusikiliza kero na changamoto za makundi mbalimbali ya ndani ya jimbo hilo ambapo amewataka kuchangamkia fursa ya uwepo wa mikopo hiyo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.
"Ninawapongeza kwa kuamua kujiunga katika kikundi, sasa niwaombe mkisajili kikundi chenu ili muweze kunufaika na mikopo ya halmashauri.
"Mpaka sasa tumeshatenga fedha nyingi za kutosha kutoka kwenye mapato yetu ya ndani kwa ajili ya mikopo tangu kusitishwa kwake na Serikali ili waweke utaratibu mzuri,"amesema Dkt.Mabula.
Katika hatua nyingine,Dkt.Mabula mbali na kupokea pongezi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya maendeleo anayoifanya kutoka kwa wanawake hao, ameahidi kuwachangia kiasi cha shilingi laki saba huku laki tano kati ya hizo ikiwa ni kwa ajili ya kutunisha mfuko wao wa kukopeshana na kuwaongezea mtaji.
Pia,alifuatilia kero ya uharibifu wa barabara ya kutoka Buswelu kupitia Kigala kufikia Buyombe.
Naye Katibu wa kikundi hicho ambaye pia ni Katibu wa Jumuiya ya UWT tawi la Kigala,Bi. Janeth Sostenes Bida mbali na kuwapongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hasan na Mbunge Dkt. Angeline Mabula kwa kazi nzuri wanazozifanya, amefafanua kuwa akina mama hao watahakikisha wanawaunga mkono katika chaguzi zijazo.