NA DIRAMAKINI
BAO pekee la Mbrazil, Yan Sasse wa Esperance Sportive de Tunis ya Tunisia dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini limeifanya klabu hiyo kujiweka nafasi nzuri kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
Mtanange huo wa nusu fainali umepigwa usiku wa Aprili 20,2024 katika dimba la Stade Olympique Hammadi Agrebi lililopo jijini Tunis, Tunusia.
Kupitia mtanange huo mkali, Sasse kutoka taifa hilo la Amerika ya Kusini alifunga bao lake la tatu la mashindano hayo barani Afrika dakika ya 41.
Ni baada ya mlinda mlango wa Mamelodi Sundowns, Ronwen Williams kupangua jaribio la kwanza la Sasse, lakini kiungo huyo alijibu upesi zaidi na kuutumbukiza mpira wavuni.
Mwaka jana Sasse alikuwa akichezea Wellington Phoenix ya nchini New Zealand kama mchezaji wa akiba kabla ya kujiunga na mabingwa mara nne wa Afrika wa Esperance.
Mamelodi Sundowns ambayo imekuwa ikilalamikiwa kuwadhulumu mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania, Yanga SC katika mechi yao ya hivi karibuni, kupitia mtanange huo ilikosa ubunifu katika kushambulia.
Aidha, ni beki wao Mothobi Mvala ambaye alikaribia kusawazisha kwa shuti kali lililokingwa kwa ustadi mkubwa na Amanallah Memmiche.