DAR ES SALAAM-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Stanbic Bank Group ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Bi. Nonkululeko Nyembezi, ambapo wamejadili fursa mbalimbali za kustawisha uchumi nchini.
Gavana Tutuba amewaeleza kuwa, Benki Kuu imeanza kutumia mfumo wa sera ya fedha unaotumia riba ya Benki Kuu katika utekelezaji wa sera ya fedha nchini ambao utaimarisha uchumi na kuwezesha mfumuko wa bei kuwa ndani ya wigo tarajiwa wa asilimia isiyozidi 5.
Ameongeza kuwa,utulivu wa sekta ya fedha na mazingira rafiki ya uwekezaji na biashara nchini unaifanya Tanzania kuwa mahali pazuri kwa wawekezaji.
Kwa upande wake, Bi. Nonkululeko Nyembezi, alieleza kufurahishwa na mwelekeo wa ukuaji wa Uchumi barani Afrika hususani Tanzania na kuahidi kutoa ushirikiano katika mikakati mbalimbali ya ukuaji jumuishi wa uchumi.
Kikao hicho kilichofanyika katika ofisi za Makao Makuu Ndogo ya BoT, Dar es Salaam, kilihudhuriwa pia na Naibu Gavana Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, Naibu Gavana Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya fedha, Bi. Sauda Msemo, Mkurugenzi Mkuu wa Stanbic Bank Group, Bw. Sim Tshabalala, Mkurugenzi Mkuu wa benki ya Stanbic Tanzania, Bw. Manzi Rwegasira pamoja na wataalamu wengine kutoka Benki Kuu.