RUVUMA-Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt.Emmanuel John Nchimbi amewaaga mamia ya wananchi, walioongozwa na viongozi wa chama na Serikali Mkoa wa Ruvuma ambao walifika Uwanja wa Ndege wa Songea kumuaga baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani humo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 13 iliyomfikisha katika mikoa sita, akianzia Katavi, kisha Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Ruvuma.
Balozi Nchimbi, ambaye katika ziara hiyo aliambatana na Issa Haji Usi Gavu, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Oganaizesheni na Amos Gabriel Makalla, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, akiwa ziarani kwenye maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo, amekagua na kuhamasisha uhai na ujenzi wa chama.
Aidha, katika ziara hiyo pia, Balozi Nchimbi ametoa maelekezo mbalimbali kwa baadhi ya viongozi na watendaji wa wizara yaliyolenga kuboresha na kuongeza kasi ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020 - 2025, hasa maeneo ya miradi ya maendeleo ya wananchi na kuwatumikia watu.
Kupitia ziara hiyo, CCM katika ngazi ya taifa, hasa kupitia kwa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, imeendeleza utaratibu wake wa kusikiliza kero za wananchi na kuzitolea maelekezo kwa ajili ya kuzitatua, huku Gavu akiendelea kuhamasisha wanachama na viongozi kuendelea kukiimarisha CCM na kujiandaa kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (2024) na Uchaguzi Mkuu (2025).