Kuvaavaa miwani kunayafifisha macho

NA LWAGA MWAMBANDE

MIAKA ya karibuni imeibuka tabia ya baadhi ya watu hususani vijana kuvaa miwani huku wengine wakidai ni kwa ajili ya kujikinga na jua.
Vivyo hivyo, wengine wamekuwa wakifanya hivyo kama ishara ya kwenda na fasheni kulingana na kikazi cha kidigitali.

Wamekuwa wakifanya hivyo, kwa kufahamu au kutofahamu kuwa, miwani ni dawa kama zilivyo dawa zingine zinazotolewa na watalaamu wa afya.

Ni baada ya mgonjwa kupimwa, hivyo hivyo miwani inapaswa kuvaliwa na mtu ambaye amepimwa macho.

Kila mmoja anatambua kuwa, matumizi ya dawa bila muongozo wa Mtaalamu wa afya zina madhara makubwa kiafya. 

Ndivyo ilivyo kwa uvaaji wa miwani bila muongozo wa daktari au Mtaalamu wa afya.

Wataalamu wa afya wanasema kuwa,kila tatizo la macho lina hatua zake, hivyo halina budi kufanyiwa marekebisho kwa miwani inayolingana na hali halisi ya kiwango cha kasoro ya uono kwa wakati huo.

Unashauriwa kuwa,kama una tatizo la kuona, kusoma au kuumia macho unapotazama mwanga, jaribu kwenda kwa mtaalamu wa macho ili akusaidie kuliko kuhatarisha macho yako kwa kubahatisha miwani mitaani.

Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anabainisha kuwa, usikubali kuyaumiza macho yako au kuwa kipofu kwa tamaa za kwenda na fasheni. Endelea;

1.Kuvaavaa miwani, bila kufanya vipimo,
Kutamba barabarani, ili tukuone wamo,
Kwamba hiyo ni fasheni, hebu sasa pata somo,
Kuvaavaa miwani, kunayafifisha macho.

2.Vijana wengi mjini, hata vijijini wamo,
Wavaavaa miwani, tena bila ya ukomo,
Hapo wenyewe wadhani, ni urembo wa kikomo,
Kuvaavaa miwani, kunayafifisha macho.

3.Elimu ya akilini, hata kichwani iwemo,
Vema kuacha utani, wavaaji usiwemo,
Usijekupata deni, nguvu macho zisiwemo,
Kuvaavaa miwani, kunayafifisha macho.

4.Kuvaa ni kizamani, kama elimu haimo,
Walokwenda darasani, na kuyapata masomo,
Ni hadi wawe shidani, ndipo wasaka vipimo,
Kuvaavaa miwani kunayafifisha macho.

5.Iwe hospitalini, au viliko vipimo,
Wachunguzwa kwa undani, kwa tatizo lililomo,
Kisha wapewa miwani, tatizo liwe ukomo,
Kuvaavaa miwani, kunayafifisha macho.

6.Mijini na vijijini, ni ufahamu uwemo,
Kusiwe mtu nyumbani, kuvaa bila vipimo,
Vema kutunza uoni, ambao shida hazimo,
Kuvaavaa miwani, kunayafifisha macho.

7.Umeikuta miwani, kuivaa kusiwemo,
Kwani wajua ya nani, aliyefanya vipimo?
Ukiitia machoni, utaparamia shimo,
Kuvaavaa miwani, kunayafifisha macho.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmailcom 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news