NA LWAGA MWAMBANDE
KWA mujibu wa wataalamu wa masuala ya hali ya hewa,mabadiliko ya tabianchi (climate change) inamaanisha mabadiliko katika wastani wa hali ya hewa duniani.
Ukizungumzia hali ya hewa hapa nchini, hapa tunaenda moja kwa moja kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).
Mara nyingi kupitia TMA utasikia kwamba kesho nyuzi joto litakuwa kiasi kadhaa, ama mvua itanyesha ama haitanyesha, vipindi vya jua vitakuwa hivi au upepo utavuma kwa kasi ya kilomita kadhaa.
Aidha,tabianchi ni hali ya hewa ya eneo fulani ambayo inapatikana kwa kutafuta wastani wake kwa muda mrefu.
Miaka ya karibuni mabadiliko ya tabianchi yamekuwa ni maumivu makubwa si tu kwa jamii bali hata kwa mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania.
Ukirejea kwa mfano Ripoti ya Kukabiliana na Pengo la Uzalishaji wa Gesi Chafu ya Mwaka wa 2021, inaonyesha kuwa, gharama za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi huenda zikaongezeka na kukadiriwa kufikia dola za Marekani kati ya bilioni 140 na bilioni 300 kwa mwaka kufikia mwaka 2030.
Vile vile gharama hizo huenda zikapanda kutoka dola za Marekani kati ya bilioni 280 na bilioni 500 kwa mwaka kufikia mwaka 2050 kwa nchi zinazoendelea pekee.
Ufadhali wa mazingira unaofanywa katika nchi zinazoendelea ili kuweka na kutekeleza mikakati ya kukabiliana na gesi chafu zilifikia dola za Marekani bilioni 79.6 mwaka 2019.
Hapo, unaweza kuona ni kwa namna gani ambapo fedha nyingi zinaweza kutumika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kiasi ambacho kama kingeelekezwa katika maendeleo kingewezesha jamii na mataifa mengi kukabiliana na umaskini.
Mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande anasisitiza ili tuweze kuyashinda haya yote yafaa kuyatunza mazingira na kuhakikisha tunafuatilia kwa umakini taarifa za hali ya hewa. Endelea;
1.Zamani nakumbukia, watu walivyozoea,
Utabiri lisikia, ila walipotezea,
Sikio yaliingia, kwingine yakatokea,
Mambo ya tabianchi, yatushikisha adabu.
2.Watu wa hali ya hewa, nani aliwazoea,
Kwamba yatatabiriwa, na yapate kutokea,
Yani toka kuzaliwa, ya kwao yalipepea,
Mambo ya tabianchi, yatushikisha adabu.
3.Ukiacha wajengaji, utabiri mezoea,
Kwamba wa kwao mtaji, usije ukapotea,
Huo wanauhitaji, miradi kuendelea,
Mambo ya tabianchi, yatushikisha adabu.
4.Sasa nani adharau, utabiri kitokea,
Tunaona angalau, wasema yanatokea,
Sasa wamepanda dau, yao tunavyopokea,
Mambo ya tabianchi, yatushikisha adabu.
5.Mvua zinazonyesha, kutwa kucha twaelea,
Hizo zimetufundisha, utabiri kupokea,
Sana imetulowesha, kufika tunalegea,
Mambo ya tabianchi, yatushikisha adabu.
6.Yanayotokea sasa, mvua kuendelea,
Hata zinaleta visa, vitu ndugu wapotea,
Yameileta hamasa, utabiri kupokea,
Mambo ya tabianchi, yatushikisha adabu.
7.Dharau hasara yako, yale yatakutokea,
Pokea faida yako, kule unakokwendea,
Huu mkubwa mwamko, kwetu wengi kupokea,
Mambo ya tabianchi, yatushikisha adabu.
8.Hali ya sasa ya hewa, ambayo yatutokea,
Kwamba tunachafuliwa, mvua kuendelea,
Hapo ndipo twaambiwa, madhara yanatokea,
Mambo ya tabianchi, yatushikisha adabu.
9.Mazingira kuharibu, ndiyo haya matokeo,
Haya ni hasa majibu, komfo kutuondolea,
Kwamba sasa tujaribu, misingi kuirejea,
Mambo ya tabianchi, yatushikisha adabu.
10.Kuyatunza mazingira, ni vema kuendelea,
Ili za sasa hasara, zisije kuendelea,
Haya sasa yatukera, yote yapate potea,
Mambo ya tabianchi, yatushikisha adabu.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602
Tags
Climate Change
Habari
Mabadiliko ya Tabianchi
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Shairi
Tanzania Meteorological Agency (TMA)