DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kati ya Julai, 2023 na Januari, 2024 Serikali imefanikiwa kukusanya sh. trilioni 17.1 ambazo ni sawa na asilimia 95.9 ya lengo la kukusanya sh. trilioni 17.9.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Aprili 3, 2024, wakati akiwasilisha Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2023/2024 na Mwelekeo wa Kazi zake kwa mwaka 2024/2025 Bungeni, jijini Dodoma.
“Katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Januari, 2024 mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia shilingi bilioni 17,188.4, sawa na asilimia 95.9 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 17,929.8 na ukuaji wa asilimia 10.0 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2022/2023.”
Amesema kati ya mapato hayo, sh. bilioni 15,159.8, sawa na asilimia 97.9 ya lengo la kukusanya sh. bilioni 15,492.7 zilikusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huku Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali zikikusanya sh. bilioni 1,374.5, sawa na asilimia 78.2 ya lengo la kukusanya sh. bilioni 1,758.3.
“Mapato yaliyokusanywa na Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia sh. bilioni 654.1 ikiwa ni asilimia 96.4 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 678.8,” amesema Waziri Mkuu.
Amewataka wafanyabiashara wote wahakikishe wanatoa risiti halali za kielektroniki za mauzo ya bidhaa na huduma wanazotoa.
“Vilevile, niwakumbushe wananchi wote kudai risiti halali za kieletroniki kila wanapofanya ununuzi wa bidhaa na huduma ili kudhibiti upotevu wa mapato na hivyo kuimarisha uwezo wa Serikali katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi ikiwemo maji, elimu na afya.”
Amesema katika mwaka 2024/2025, Serikali itaendelea kuweka vipaumbele zaidi kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa bajeti kwa kuimarisha na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuwianisha, kufuta au kupunguza viwango vya kodi, tozo na ada zinazoonekana kuwa kero.
Pia itaboresha mazingira ya ulipaji kodi na kuongeza wigo wa kodi; kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi; na kuimarisha na kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA ya ukusanyaji wa mapato.
“Hatua hizi zitawezesha kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kukuza mapato ya ndani kufikia asilimia 15.7 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 15.3 mwaka 2023/2024,” amesema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema kati ya Julai, 2023 na Februari 2024, miradi 416 ilisajiliwa kwenye Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kupitia mifumo ya kusajili miradi.
Amesema,miradi ya Watanzania ni 153, wageni ni 175 na ubia ni 88, sawa na ongezeko la asilimia 205 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2022/2023 ambapo jumla ya miradi 203 ilisajiliwa.
“Miradi hiyo inatarajia kuwekeza jumla ya dola za Marekani milioni 4,490 na kuzalisha ajira 119,717. Uwekezaji huo utaimarisha uchumi wa Taifa pamoja na kuboresha maisha ya watu kupitia fursa za ajira, ukusanyaji wa mapato na kunufaika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya jamii,” amesema.
Katika kipindi cha mwaka 2024/2025, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuhamasisha ushiriki wa Halmashauri na Serikali za Mikoa, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika uendelezaji wa maeneo ya uwekezaji na uendelezaji wa miundombinu ili kuvutia uwekezaji; na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wawekezaji katika ngazi zote kwa kuanzisha benki ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji mahususi.
Kwa mwaka 2024/2025, Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe sh. 350,988,412,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 146,393,990,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 204,594,422,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.
Pia ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh. 181,805,233,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 172,124,423,000/- ni za matumizi ya kawaida na sh. 9,680,810,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.