PWANI-Mbunge wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani na Naibu Waziri wa Utumishi na Utawala Bora,Mhe. Ridhiwani Kikwete ameshiriki kwenye uzinduzi wa Jukwaa la kuwezesha wanawake kiuchumi Kata ya Kiwangwa, Tarafa ya Msata.
Sherehe hizi zilipambwa na maandamano ya amani, kujadili uwezeshaji na fursa mbalimbali za kumkomboa na kumuwezesha mwanamke katika jamii.
Kupitia fursa mbalimbali zilizopo zikiwemo za ndani ya halmashauri na zile zinazosimamiwa na Serikali Kuu wanawake wana nafasi ya kusaidia ukuaji wa kipato ndani ya jamii na familia.
Kwa mujibu wa taarifa za Sensa, ongezeko wa idadi ya wanawake wanaotegemewa ndani ya familia umeongezeka kufikia asilimia 37.6.
Idadi hii inatoa fursa za kuwezesha wanawake katika jamii.
Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwemo kurudisha mikopo ya asilimia 10, mfuko kusaidia Wananchi kuendelea kutenga fedha kuwezesha wananchi kiuchumi na fursa nyenginezo.
Katika mkutano huo, Ofisi ya Mbunge Ridhiwani ilichangia shilingi milioni 4.6 kuwezesha vikundi vya Wanawake Kiwangwa kukopeshana.