KAGERA-Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Mhe. Stephen Byabato amegawa kadi 18 za Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa kwa watu wa makundi maalum Kisiwani Musira kilichopo Kata ya Miembeni Jimbo la Bukoba Mjini mkoani Kagera.
Byabato amesema zoezi hilo ni endelevu ambapo watu wa Makundi Maalum wakiwemo Walemavu na Wazee takribani 140 katika kata zote za Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wanatarajia kupata bima ili kuwasaidia kupata huduma za afya kwa urahisi kwenye vituo vya Serikali pale watakapokuwa na uhitaji wa huduma hiyo.
Ameongeza kuwa kadi za Bima ya Afya zitatolewa kwa wananchi kumi kutoka kila kata ndani ya jimbo hilo.
Wananchi wa Kisiwa cha Musira waliopata bima hizo wamemshukuru Mbunge Byabato kwa kuwapa msaada huo na kukiri kuwa bima hiyo ni mkombozi kwao katika kupata huduma stahiki za afya.
Wamesema wakati mwingine walikuwa wanapata changamoto ya kupata huduma za afya kwa kuwa walikuwa hawana fedha hivyo Bima hizo zitawasaidi sana.
Awali, Bi. Juleth Richard, akisoma risala iliyoandaliwa na Mwenyekiti wa Mtaa wa Musira, amesema kuwa katika mtaa huo yapo mambo mengi ambayo yamefanyika ikiwa ni pamoja na ujenzi wa choo, Boti ya Mv Byabato na majiko ya gesi kwa mama na Baba lishe.
Baada ya kufika kisiwani hapo Mbunge Byabato akiwa ameambatana na kamati ya maandalizi ya shughuli hiyo, wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka Jimbo la Bukoba Mjini na wajumbe kutoka group la Whatsapp la Bukoba Mjini Mpya walifanya shughuli mbalimbali ikiwemo kupanda miti kwa ajili ya kutunza mazingira.