NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, katika kipindi cha robo ya kwanza, mikopo chechefu imeendelea kupungua hadi kufikia asilimia 4.5 ikiwa ni lengo nzuri ikilinganishwa na asilimia 5 ambayo walikuwa wamejiwekea.
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba ameyasema hayo leo Aprili 4,2024 katika ofisi ndogo za makao makuu ya Benki Kuu jijini Dar es Salaam mbele ya wakuu wa taasisi za fedha na vyombo vya habari.
Ni wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ambayo imetangaza ongezeko la Kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kutoka asilimia 5.5 hadi asilimia 6.
Uamuzi huo umefikiwa wakati wa kikao cha MPC kilichofanyika Aprili 3, 2024 kwa kuzingatia tathmini ya mwelekeo wa uchumi iliyofanyika mwezi Machi,mwaka huu.
Riba hiyo mpya itatumika katika kipindi cha robo ya pili kuanzia leo Aprili 4,2024 hadi Juni, mwaka huu.
Utekelezaji wa Sera ya Fedha kwa kutumia Mfumo wa Riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate) ulianza Ijumaa ya Januari 19, 2024 ambapo BoT iliachana na mfumo uliokuwepo wa Ujazi wa Fedha.
Katika robo ya kwanza ukomo wa riba ulikuwa asilimia 5.5 kati ya BoT na benki za biashara ili kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
"Kwa hiyo tumefanya vizuri zaidi na kuhakikisha watu wengi wanachukua mikopo na wanatekeleza shughuli zao na kurejesha.
"Ikiwa ni moja wapo ya kiashiria cha mazingira mazuri ya ufanyaji biashara nchini,ambaoo watu wanaweza wakakopa wakafanya biashara na kurejesha kwa wakati,"amefafanua Gavana Tutuba.
Pia, amesema Sekta ya fedha kwa ujumla imeendelea kuwa imara ikiwa na mtaji wa kutosha, ukwasi wa kutosha na inaendelea kuhimili changamoto na misukosuko inayojitokeza duniani.
"Kwa Tanzania tumeendelea kuwa na uhimilivu mzuri kwenye sekta ya fedha na imeendelea kukuwa kwa kiwango kizuri na imeendelea kutoa mikopo ambapo utoaji wa mikopo kwa sekta binafsi umekuwa kwa asilimia 17.
"Kiwango ambacho ni kizuri ukilinganisha na mazingira yaliyopo hali ambayo inachochea kuendelea kutoa mchango mkubwa kwenye sekta binafsi."