Mliberia jela miaka 20, faini shilingi milioni 200 kwa kusafirisha dawa za kulevya Dar

DAR ES SALAAM-Mahakama ya Rufani imethibitisha kifungo cha miaka 20 jela na faini ya zaidi ya milioni 200 aliyoamriwa Mliberia, Edwin Cheleh Swen kulipa kwa kusafirisha kete 97 zenye uzito wa gramu 1509.35.
Picha haina uhusiano na habari hii. (Kwa hisani ya Mtandao).

Ni za dawa ya kulevya aina ya heroine katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Majaji Winfrida Korosso, Sam Rumanyika na Leira Mgonya walifikia uamuzi huo hivi karibuni baada ya kutupilia mbali rufaa ambayo mrufani Swen alikata kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, iliyosikiliza kesi ya uhujumu uchumi.

Wakati wa kusikilizwa kwa rufaa hiyo, wakili wa mrufani alipinga, miongoni mwa mambo mengine, kupokelewa kwa dawa hizo, akidai kuwa hazikujadiliwa katika shauri la muhamisho (commital proceedings) kama inavyotakiwa kisheria.

Baada ya kupitia kumbukumbu za rufaa hiyo, majaji hao walibaini kuwa mrufani alifahamishwa wakati wa shauri hilo kuwa vielelezo hivyo halisi vitatolewa mahakamani katika kesi hiyo.

“Hivyo, mrufani alifahamishwa ipasavyo na akapewa fursa ya kujua na kuelewa mapema kiini cha kesi hiyo ili kumwezesha kujitetea. Kwa hiyo, tunakubaliana na upande wa mashtaka kwamba lalamiko hili halina msingi,” walisema.

Mrufani huyo pia alilalamikia usahihi wa hukumu hiyo kwa kuwa wakati akitoa hukumu dhidi yake jaji aliyesikiliza kesi hiyo alishindwa kuzingatia miaka tisa na miezi mitano aliyokaa rumande kinyume na kifungu cha 172 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Baada ya kutafakari hoja zilizowasilishwa, majaji hao walibainisha kuwa mahakama hiyo iliendelea kumtia hatiani mrufani hadi kifungo cha miaka 20 jela, kifungo cha chini zaidi kwa kupatikana na hatia na suala la malalamiko yake lilizingatiwa.

Kulikuwa na malalamiko mengine kuhusiana na mlolongo wa uhifadhi wa dawa za kulevya ambazo zilikamatwa kutoka kwa mrufani kwamba zilichakachuliwa kutoka uwanja wa ndege hadi Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kabla ya kuwasilishwa mahakamani kama kielelezo wakati wa kesi.

Baada ya uchunguzi wa kina wa ushahidi huo, majaji hao walijiridhisha kuwa ushahidi unaonyesha kuwa wakiwa chini ya uangalizi katika uwanja wa ndege, akituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya, mrufani alijisaidia haja kubwa kete 97 ambazo zilikubaliwa kama vielelezo.

“Ushahidi unaeleza wazi ukweli huu kwamba vidonge vilivyotolewa kwa njia ya haja kubwa vilivyokamatwa kwa tarehe na muda uliotajwa baadaye vilioshwa, kuwekwa kwenye mifuko nyeusi na kuhifadhiwa kwenye droo ya ofisi na (maofisa wa polisi) ambao walikuwa walinzi pekee wakati wa zamu zao za kazi ," walisema.

Majaji hao walisema kwa kuchukua ushahidi huo kwa ujumla hatua kwa hatua, walijiridhisha kuwa ushahidi wa mdomo wa mashahidi wa upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa vidonge hivyo viliwekwa chini ya ulinzi kwenye droo za Ofisi za Kitengo cha Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (ADU) katika uwanja wa ndege.

Walibainisha kuwa dawa hizo wakati wote zilikuwa chini ya ulinzi wa maafisa wa polisi na kwamba hakuna nafasi au hatari ya kuathiriwa kabla ya kukabidhiwa kwa kiongozi mwandamizi wa polisi.

"Matokeo yetu yanaimarishwa zaidi na ukweli kwamba fomu za uchunguzi zilizotiwa saini na mashahidi, mrufani (na maafisa wawili wa polisi) zinaonyesha wazi idadi ya vidonge vilivyochukuliwa kwa kila tukio," majaji walisema.

Pia walitambua ukweli kwamba uaminifu wa mashahidi ulithibitishwa na jaji wakati wa kusikiliza kesi, na hawakuona chochote cha kutowaamini.

"Kinachotuongoza ni ufahamu wetu kwamba kila shahidi ana haki ya kuthibitishwa na kuaminiwa," walisema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news