NJOMBE-Mtendaji wa Kata ya Ninga katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe mkoani Njombe, Lavenda Meshack Nyagori amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Njombe kwa tuhuma za kuomba rushwa.
Aprili 9, 2024 mtuhumiwa huyo alifunguliwa kesi ya jinai kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa kinyume na Kifungu cha 15 (1)(a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (cap 329 Re 2022).
Ilidaiwa,mshtakiwa akiwa Mtendaji wa Kata ya Ninga, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, aliomba rushwa kiasi cha shilingi 120,000 kutoka kwa Bw.Joel Daniel Kuyava na kupokea kiasi cha shilingi 100,000.
Lengo ni ili amsaidie kutatua mgogoro wa kifamilia ya mwanaye Samson Joel Kuyava na mkewe Atira Lutumo.
Akisomewa mashtaka hayo mbele ya Mhe. Romanus Mlowe ambaye ni Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Njombe, mshtakiwa alikana makosa yote.
Mshtakiwa alipewa dhamana na alishindwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo yupo ndani na shauri limepangwa kusikilizwa tena Aprili 22, 2024.