ARUSHA-Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umekutana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kujadili maboresho ya huduma za matibabu yaliyofanyika ikiwemo Kitita cha Matibabu cha mwaka 2023.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Bw. Bernard Konga, amefafanua manufaa ya Kitita cha mafao kwa wanachama wa Mfuko huo ikiwemo ongezeko la dawa mpya 254 ambazo awali hazikuwemo.
"Kitita hiki kipya kimetatua changamoto ya wanachama kukosa baadhi ya dawa na huduma kwa kuwa kimejumuisha huduma nyingi ambazo kwenye kitita cha mwaka 2016 hazikuwemo"
Aidha,amesema kitita hiki kimesogeza huduma za kibingwa na ubingwa bobezi karibu na wananchi kuanzia hospitali za ngazi ya Mkoa na Kanda hatua inayoondoa usumbufu wa kukosa baadhi ya dawa na huduma nyingine.
Maboresho haya pia yamelenga kuwalinda wanachama kuendelea kutumia dawa zisizo na matokeo chanya hivyo kuwaepusha na magonjwa sugu yasiyoambukiza.
Kutokana na hayo, amewahakikishia viongozi hao kuwa kitita hicho kimezingatia mahitaji halisi ya huduma zinazohitajika kwa sasa.
Bw. Konga alitumia fursa hiyo kuliomba Shirikisho hilo kuendelea kushirikiana na waajiri hususan katika kuwahamasisha kuwasilisha michango kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa kukosa huduma.
Kwa upande wa TUCTA, ulioongozwa na Rais wake Bw. Tumaini Nyamhokya alitoa rai kwa NHIF kuhakikisha unashirikiana na vyama vya wafanyakazi katika hatua mbalimbali za maboresho ya huduma kwa kuwa ndio watumiaji wakubwa wa huduma za mfuko.
Aidha,ameupongeza Mfuko kwa maboresho ambayo yamefanyika kwenye kitita ikiwemo nyongeza ya dawa na huduma ambazo awali hazikuwemo pamoja na kushusha huduma ngazi ya chini itakayosaidia wanachama kupata huduma kwa urahisi zaidi.