Njooni mkawekeze kwenye madini muhimu na mkakati-Waziri Mavunde

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imesema, jitihada mbalimbali zimeendelea kufanyika kuhakikisha madini muhimu na madini mkakati yananufaisha Taifa huku ikiwakaribisha wawekezaji mbalimbali kuwekeza katika madini hayo.
Hayo yamesemwa leo Aprili 30, 2024 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Amesema, jitihada hizo ni pamoja na kufanya tafiti na kutangaza fursa za uwepo wa madini nchini kupitia maono ya Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri.

Pia, amesema suala la madini muhimu na madini mkakati ni miongoni mwa maboresho yaliyopendekezwa kufanyika katika Sheria ya Madini, Sura 123 kupitia muswada wa marekebisho ya Sheria mbalimbali namba 4 wa Mwaka 2024 ambao ulisomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa 14 wa Bunge.

"Lengo la maboresho hayo ni kuweka usimamizi thabiti wa madini mkakati na madini muhimu ili kupata manufaa mapana kupitia mnyororo wa thamani wa madini hayo."

Waziri Mavunde amesema, kwa kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi Machi 2024, leseni ya Uchimbaji Mkubwa wa Madini ya Heavy Mineral Sands imetolewa kwa Kampuni ya Nyati Mineral Sands Limited (NYSL) katika mradi wa Tajiri uliopo Wilaya ya Pangani mkoani Tanga.

Vile vile, leseni ya usafishaji madini imetolewa kwa kampuni ya Tembo Nickel Refining Company Limited uliopo Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Amesema,thamani ya uwekezaji katika miradi hiyo inatarajiwa kuwa jumla ya dola za Marekani milioni 760.23 sawa na shilingi trilioni 1.78.

"Uwekezaji huu utaongeza ajira, kodi, tozo mbalimbali, manufaa yatokanayo na uwajibikaji wa kampuni za madini kwa jamii (CSR) na ushirikishwaji wa watanzania katika uuzaji wa bidhaa na utoaji huduma katika shughuli za madini na uhawilishaji wa teknolojia kwa watalaam wa kitanzania."

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mavunde amesema, Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika madini muhimu na mkakati ili madini hayo yaweze kunufaisha Taifa kutokana na uhitaji wake kwa ajili ya teknolojia mbalimbali pamoja na kupunguza hewa ya ukaa duniani.

Amesema, kutokana na uhamasishaji huo,wizara imeendelea kupokea maombi mbalimbali ya uwekezaji kwenye madini hayo ikiwemo ombi la leseni ya uchimbaji wa madini ya kinywe la Kampuni ya Duma Tanzgraphite Limited (DTL) katika eneo la Epanko, Wilaya ya Ulanga.

"Kwa kuwa kuna uhitaji mkubwa wa madini hayo duniani kwa sasa, nachukua fursa hii kuwakaribisha wawekezaji kuendelea kuwekeza nchini kwenye utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji na uongezaji thamani pamoja na biashara ya madini nchini hususani kwenye madini muhimu na mkakati,"amesisitiza Waziri Mavunde.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news