MOROGORO-Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amewataka Watumishi wa Wizara hiyo kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi na kwa wakati ikiwa ni pamoja na kuwahudumia ipasavyo wateja wao kwa kutumia mifumo iliyopo.
Prof. Nombo ametoa rai hiyo Aprili 24, 2024 Mkoani Morogoro, wakati akizungumza katika Ufunguzi wa Mkutano wa 33 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara huku akisisitiza Watumishi wote kutoa huduma bora kwa wateja.
‘’Kila mdau wa Elimu ana haki ya kuhudumiwa kwa wakati, tukitekeleza hilo itatusaidia Taifa letu kuwa na watanzania walioelimika, wenye ujuzi na maarifa ya kulipeleka Taifa letu katika ushindani wa Sayansi, Teknolojia,"amesema Prof. Nombo.
Amesema, Serikali imedhamiria kufanya mageuzi katika Sekta ya Elimu nchini, na sasa imeanza kutekeleza Sera ya Elimu 2014 Toleo la 2023 na Mitaala iliyoboreshwa na kazi ya kutoa Mafunzo endelevu Kazini kwa Walimu wa Madarasa ya Awali, Msingi, Sekondari (Amali) pamoja na Wathibiti Ubora wa Shule na Viongozi wanaosimamia Elimu inaendelea.
Wakati huo huo amewataka Wajumbe wote wa waendelee kuzingatia Waraka wa Elimu Na. 24 wa Mwaka 2002 unaohusu adhabu ya viboko na kwamba wawe wa kwanza kutoa taarifa juu ya ukiukaji unaofanyika ikiwemo ukiukwaji wa maadili, mila na tamaduni za mtanzania katika Taasisi za kielimu.
Akizungumza Afisa Elimu Kazi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijaa, Ajira na Wenye ulemavu,Bi. Honesta Ngowi ameipongeza Wizara ya Elimu kwa kuwa mfano katika utekelezaji wa Sera za ushirikishwaji wa Wafanyakazi sehemu za kazi, ambapo ni miongoni mwa Wizara chache, zenye mabaraza yaliyoundwa na chama zaidi ya kimoja, na kukiwa utulivu na ushirikiano baina ya vyama na menejimenti.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE),Bw. Moshi Kisinga amesema Mkutano huo hufanyika kulingana na mikataba iliowekwa.
Kisinga amesisitiza kuwa wajibu huo unatekelezwa kwa umoja katika kuhakikisha kutetea maslahi ya Wafanyakazi.