DODOMA-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema,viongozi na Watanzania wanajifunza mengi kutokana na historia ya utendaji kazi wa Mzee John Samwel Malecela.
Ni katika nyadhifa mbalimbali alizoshika serikalini na Chama Cha Mapinduzi na ataendelea kuwa hazina muhimu ya maarifa na uzalendo hapa nchini.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo Aprili 21,2024 katika sherehe za Kumbukizi ya miaka 90 ya kuzaliwa Mhe.Mzee John Samwel Malecela, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyika nyumbani kwake Uzunguni jijini Dodoma.

Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, Watanzania wataendelea kufaidika na busara, hekima, na ushauri wake katika kuiletea maendeleo nchi yetu na uzoefu wake mkubwa alionao Mzee Malecela katika uongozi, siasa na diplomasia ya Kimataifa.

