ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema ni wajibu kuulinda Muungano, kuuendeleza, kuudumisha na kuimarisha zaidi ili kuzidi kunufaika kwa dhamira ile ile ya Waasisi wa Taifa letu.
Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa umoja wa Watanzania unazidi kuimarika , ushirikiano katika shughuli mbalimbali unaongezeka na amani inaendelea kudumu nchini.

Aidha, Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote zinazojitokeza katika utekelezaji wa masuala ya Muungano.
Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka vipaumbele masuala ya kuimarisha Muungano.
Rais Dk.Mwinyi amesema hayo Aprili 14,2024 alipofungua Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Maonesho ya Taasisi mbalimbali viwanja vya Nyamanzi , Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rais Dk.Mwinyi amesema Tanzania imefikia mafanikio makubwa kipindi cha Miaka 60 katika nyanja zote za maendeleo ya kisiasa, kiuchumi na huduma za jamii.

Rais Dk.Mwinyi amesema kipindi cha miaka mitatu, 2021 hadi mwaka 2024 hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwepo.
Vilevile Rais Dk.Mwinyi amesema Tanzania imeendelea kubaki katika historia na mfano bora wa kudumisha Muungano barani Afrika na Duniani kote.