NA PETER JOSEPH
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 23 Aprili 2024 atakuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 38 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) utakaofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip mjini Zanzibar.
Mkutano huo utakaofanyika kuanzia tarehe 23 Aprili, 2024 na kukamilika tarehe 25 Aprili, 2024 utawakutanisha washiriki 600, wakiwemo Wastahiki Mameya wa Majiji na Manispaa, Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri, na Wakurugenzi wa Halmashauri zote 184 za Tanzania Bara.
Kaimu Katibu Mkuu wa ALAT Taifa Bw. Mohamed Maje amesema maandalizi yote muhimu kwa ajili ya kufanyika kwa mkutano huo yamekamilika.
Amesema pamoja na mambo mengine, mkutano huo ni fursa ya kuwakutanisha viongozi wakuu wa Serikali Kuu na za Mitaa kwa ajili ya kutoa maelekezo na miongozo ya kisera kwa watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini.
Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni Jambo Letu; Shiriki kwa Maendeleo ya Taifa”
Rais wa Zanzibar Mhe.Dkt Hussein Mwinyi anatarajia kufunga Mkutano huo tarehe 25 Aprili, 2024.