Safari mpya ya Salim Kikeke ndani ya CROWN Media, mpambanaji asiyekata tamaa

NA GODFREY NNKO

IKIWA ni takribani mwaka mmoja tangu astaafu utumishi wake wa miaka 20 ndani ya Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), mtangazaji mbobezi ndugu Salim Kikeke na kurejea nchini, hatimaye kipaji chake kimehitajika tena ndani ya Crown Media.

Kituo hicho cha habari kilichopo jijini Dar es Salaam kinamilikiwa na msanii wa Bongo Flava, Ali Saleh Kiba maarufu kama Alikiba.

Ndugu Kikeke ambaye ni Mtanzania aliaga rasmi BBC Aprili 28, 2023 wakati akitamatisha kipindi maarufu zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki cha Dira ya Dunia na kusema kuwa, anakwenda kufanya majukumu mengine ingawa hakuyaweka wazi.

Aidha, kupitia ukurasa wa Afisa Mtendaji Mkuu wa Crow Media, Alikiba tarehe 29,2024 ameandika,"Hapa ni nyumbani,karibu Mfalme wa habari, karibu unapostahili zaidi, Mfalme kakutana na Mfalme.

“My brother Salim Kikeke hii ilikuwa ndoto na maono tuliyokuwa nayo muda mrefu. Wakati unafanya maamuzi ya kurudi nyumbani Tanzania tulipata nafasi ya kuzungumza na nikakueleza kiu yangu ya kutaka kufanya kazi na wewe gwiji, nguli na mtaalam wa tasnia hii ya habari Afrika na Dunia.
"Najua simu zilikuwa nyingi sana, lakini uliona Crown ni sehemu sahihi sana kwako. Karibu kuwa sehemu ya historia tunayoenda kuiandika pamoja.

"Nimekuvisha taji na Crown Media tunaamini hesabu zetu za kimkakati zimekaa sawa. Karibu sana nyumbani."

Kwa upande wake ndugu Salim Kikete baada ya kujiunga na CROWN Media ameandika,

"Kwa heshima kubwa na taadhima nachukua nafasi hii kutangazia umma kujiunga rasmi na familia ya Ufalme.

"Huu ni ushirika ambao haujapata pengine kutokea kuunganisha majina makubwa katika sanaa na katika habari.

"Tunaunganisha nguvu katika kupeleka mbele tasnia zetu. Huu ni mwanzo wa safari ndefu ya na kusisimua katika kuleta mapinduzi kwenye habari na muziki.

"Nimerudi nyumbani Tanzania kwa ajili ya jambo hili. Hapa ni nyumbani. Karibuni sana. Karibuni nyote kwenye Ufalme."

Salim Kikete

Ndugu Kikeke ni kati ya vijana wa Kitanzania ambao wanaonekana kupambana hadi kuweza kujenga majina na heshima zao duniani bila kukata tamaa.

Hivi karibuni alinukuliwa na vyombo vya habari vikieleza kuwa, baada ya kumaliza Stashahada ya Umwagiliaji katika Chuo cha Kilimo Nyegezi, Mwanza alikutana na changamoto kadhaa hasa ya kukosa ajira kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu mfululizo.

”Nilimaliza Stashahada yangu mwaka 1994 kozi ya Umwagiliaji, kwa sasa labda ningekuwa bwana shamba au mfanyakazi wa kilimo,” anasema Kikeke.

Baada ya kumaliza chuo, juhudi za kusaka ajira zilikuwa ngumu.Kwa karibu mwaka mzima wa 1995, alikwenda katika machimbo ya Tanzanite ya Mererani Arusha. “Hakukuwa na ajira na kishawishi cha kujiingiza katika uhalifu kilikuwa kikubwa,” anasema bila kueleza zaidi.

Katika hatua ya kuepuka mazingira hayo aliamua kuwa ‘Mwanaapolo’ kama wanavyojulikana wachimbaji wa Tanzanite yaani kutumika kuingia kwenye mashimo kubeba mizigo au kazi nyingine migodini. Baada ya kushauriwa na mama yake kuondoka mchimboni, alirejea Dar es Salaam.

Aidha, katika kipindi hicho Kikeke anasema alikuwa akishinda kijiweni mitaa ya Sinza Kumekucha akiwa na rafiki yake, Joseph Mboya ambaye kwa sasa ni marehemu.

“Mboya ndiye mmoja kati ya rafiki zangu ambao tulibadilishana mawazo, tulifarijiana na kufikiria matarajio ya ndoto zetu, mambo yalikuwa magumu mpaka nikafikia hatua ya kusema basi imetosha,” anasema Kikeke.

Kuingia utangazaji

Mara baada ya kuona matumaini yakififia kupitia taaluma yake ya kilimo, Kikeke aliamua kubadilisha ukurasa wa maisha baada ya kupiga hodi katika ofisi za kituo cha TV cha CTN ambacho kilikuwa na redio wakati huo ikijulikana kama Classic FM ambayo kwa sasa ni Magic FM.

Sababu, nia na ujasiri wa kuchukua uamuzi huo, haikutokea kama ajali, bali ilitokana na ushawishi aliokuwa ameupata kutoka kwa mama yake mzazi ambaye ni marehemu kwa sasa.

“Mama yangu alikuwa wa kwanza kunijengea uwezo wa kuingia katika utangazaji, alikuwa anapenda sana kusikiliza habari za redioni na alinishawishi kufuatilia kila habari iliyokuwa inaendelea duniani, nikawa na uwezo wa kutamka maneno vizuri na kusoma habari,” anasema Kikeke.

Ilikuwa ni mwishoni mwa 1997, Kikeke alifika katika ofisi za kituo cha kurusha matangazo cha CTN. “Kwa sasa wanaita Magic FM, walikuwa wanafungua kituo kipya cha Classic FM hivyo niliomba kufanya kazi bure, nikapewa kipindi cha kucheza miziki ya Kiingereza,” anasema Kikeke.

Anasema, baada ya kupata uhakika wa kuendelea na kazi hiyo, Januari mwaka 1998 aliamua kwenda kusoma kozi fupi ya utangazaji habari katika chuo cha uandishi wa habari cha Tanzania School of Journalism (TSJ).

”Pale nilisoma cheti kwa miezi mitatu na kurudi tena kazini, nikaanza kusoma habari za Kiingereza na Kiswahili wakati mwingine nilikuwa naenda kutafuta habari. Hata hivyo mwezi mmoja baadaye wakanifukuza kazi kwa sababu ambazo nisingependa kufafanua zaidi,” anasema.

Kikeke baada ya kufukuzwa kazi, hakuishia kulia mtaani, badala yake alianzisha mkakati wa kusaka ajira tena kwenye taasisi yenye hadhi ya juu zaidi, Radio Tanzania (RTD) ambayo sasa ni Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), hiyo ilikuwa ni mwishoni mwa mwaka 1998.

”Kwa kipindi hicho Abdul Ngarawa alikuwa mkurugenzi wa RTD, nikapelekwa idhaa ya Kiingereza, ‘English Service’, na kuandaa vipindi vya muziki kila siku kuanzia saa 12:00 jioni mpaka saa 6:00 usiku,” anasema Kikeke na kufafanua kuwa alikuwa akifanya kazi kwa muda ‘part-time.

Alianza kupangiwa vipindi vya kutangaza baada ya kukaa kwa zaidi ya mwaka mmoja. “Baadaye nikapewa kipindi cha Mwelekeo kilichoanzishwa wakati wa maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, nilikuwa mtangazaji wa mwanzoni kabisa katika kipindi hicho,” anasema Kikeke.

Katika kipindi hicho, Radio Tanzania walianzisha kituo cha matangazo cha FM, kiitwacho PRT kikitoa matangazo kwa lugha ya Kiingereza.

RTD na Kituo cha PRT ndizo kwa sasa zinafahamika kama TBC na TBC1. “Mimi nikaondoka pale na kurudi tena CTN,” anasema.

Baada ya kurudi katika kituo hicho, Kikeke alifanikiwa kupata nafasi ya kusoma habari kwenye TV mpaka mwezi Agosti wakati kampuni hiyo ilipouzwa na kuwa chini ya kituo cha Channel Ten na DTV. Baadae alihamia ITV.

Aidha, baada ya hapo alifanikiwa kuandika barua ya maombi ya kazi katika Kituo cha Radio One. “Kwa wakati huo Charles Hilary ndiye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Radio One, akaniomba nimpatie mfano (Demo) ya kipindi chochote nilichowahi kufanya, kwa bahati mbaya sikuwa na ya radio ila nikawa na ya TV,”anasema Kikeke.

Anaongeza kuwa, hali hiyo ikamfanya abadilishe mlango wa kutoka Redio One na kuingia ITV. “Charles Hilary akaipeleka ile demo upande wa televisheni ya ITV, kulikuwa na Betty Mkwasa na Joyce Mhaville, wakaipenda kazi yangu na kuagiza niripoti pale kazini,”anasema.

Kikeke alipangiwa jukumu la utangazaji wa vipindi vya taarifa za habari kila siku na habari za ‘Jiji Letu’ hata hivyo mambo yalibadilika kwa muda mfupi pale ofisini.

Safari ya BBC

Radio One walikuwa ni Redio washirika wa BBC hivyo walikuwa na mkataba wa kuchukua mtangazaji mmoja kila mwaka na kumpeleka kufanya kazi makao makuu ya BBC kwa muda wa miezi kadhaa.

"Mwezi Mei 2003 nikafaulu majaribio ya kuingia BBC," ambako amehitimisha majukumu yake tayari baada ya kuaga wafuasi wake Aprili 28, 2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news