NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde amesema, mwenendo wa mapato ya fedha za kigeni kupitia Sekta ya Madini umekuwa ukiimarika mwaka hadi mwaka.
Ameyasema hayo leo Aprili 30, 2024 wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma, hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025
Waziri Mavunde amesema, mwaka 2023 madini yenye thamani ya dola za Marekani milioni 3,551.4 yaliuzwa nje ya nchi sawa na asilimia 56.2 ya mauzo ya bidhaa zisizo za asili (non traditional goods).
Hiyo ni ikilinganishwa na mauzo ya dola za Marekani milioni 3,395.3 sawa na asilimia 56.0 mwaka 2022.
"Hivyo, mauzo ya madini ya mwaka 2023 yaliongezeka kwa dola za Marekani milioni 156.1 ambayo ni asilimia 4.6 kutoka mauzo ya mwaka 2022. 39."
Mbali na hayo,Waziri Mavunde amesema, katika kuhakikisha kuwa mchango wa Sekta ya Madini katika kuliingizia taifa fedha za kigeni unaongezeka, wizara itaendelea kusimamia utekelezaji wa matakwa ya kifungu cha 10 cha Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusu Umiliki wa Utajiri Asilia na 36 37 Maliasilia za Nchi, Sura ya 449.
Ni kinachoweka sharti la mapato yatokanayo na uvunaji wa maliasilia za nchi ikiwemo madini kuwekwa katika taasisi za fedha zilizopo nchini.
Aidha, amesema wizara inaendelea kushirikiana na mamlaka nyingine za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika kuhakikisha kuwa malipo ya mauzo ya madini yaliyofanyika nje ya nchi yanarejeshwa nchini.
"Lengo ni kuhakiki kama malipo hayo yamefanyika na kuhifadhiwa kwa kuzingatia masharti ya Kanuni za Fedha za Kigeni za Mwaka 2022.
"Nitoe wito kwa wachimbaji na wafanyabiashara ya madini kuzingatia sheria na kanuni zinazoelekeza kufungua akaunti katika taasisi za kifedha zilizopo nchini na kurejesha fedha za mauzo ya madini yaliyofanyika nje ya nchi katika akaunti hizo."
Pia,Mheshimiwa Waziri Mavunde amesema, katika mwaka 2023, jumla ya vibali 11,258 vya kuuza madini nje ya nchi vilitolewa ikilinganishwa na vibali 10,318 vilivyotolewa mwaka 2022.
Amesema, ongezeko la vibali hivyo kwa kiasi kikubwa limetokana na kuongezeka kwa uhitaji wa madini ya vito na makaa ya mawe nje ya nchi.
"Aidha, katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, jumla ya vibali 115 vya uingizaji madini nchini vilitolewa ikiwa ni hatua mojawapo ya kusimamia na kudhibiti biashara ya madini nchini."
Kuhusu, mwenendo wa mapato ya kodi yatokanayo na Sekta ya Madini, Waziri Mavunde amesema, umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.
Mwaka 2022/2023 amesema, mapato ya kodi 17 18 yatokanayo na Sekta ya Madini yalifikia shilingi 3,143,212,216,996.76 sawa na asilimia 13.9 ya mapato yote ya kodi yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Waziri Mavunde amesema,mapato hayo yameongezeka kwa asilimia 50.3 kutoka shilingi 2,091,256,445,986.27 mwaka 2021/2022.
Ombi
Mheshimiwa Waziri Mavunde ameliomba Bunge liridhie na kupitisha makadirio ya shilingi 231,983,614,000.00 kwa ajili ya matumizi ya wizara na taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Kati ya fedha hizo shilingi 140,661,200,000.00 sawa na asilimia 60.63 ya bajeti yote ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Aidha, shilingi 91,322,414,000.00 sawa na asilimia 39.37 ya bajeti yote ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Huku kati ya fedha hizo, shilingi 24,872,875,000.00 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi (PE) na shilingi 66,449,539,000.00 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC) ya wizara na taasisi zilizo chini yake.
Tags
Akiba Fedha za Kigeni
Anthony Mavunde
Bunge la Bajeti
Habari
Sekta ya Madini Tanzania
Wizara ya Madini