SINGIDA-Serikali inaendelea kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali katika maeneo muhimu yanayoigusa jamii ikiwemo Afya, Elimu na Miundombinu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha na Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) alipokuwa akizungumza na wananchi wa kata ya kyengege, Wilayani Iramba, alipofanya Mkutano na Wananchi wa Kata hiyo kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zao na kuwaeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya miaka mitatu tangu Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan aingie madarakani.
"Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mambo makubwa na yanayoonekana kila kona ya nchi, Miradi ya kimkakati inakamilika yote, miradi mipya imemwagika kila sekta, ukienda kwenye Afya amejenga vituo vikubwa kila Tarafa, Ujazilizi wa Umeme vijijini unaendelea, Barabara za kisasa zinajengwa kila kona, Madarasa yamejengwa ya kutosha upande wa Elimu Msingi na Sekondari."
"Niwahakikishie Rais anayo nia ya dhati ya kuleta mabadiliko katika nchi yetu na tumeshuhudia pia upande wa Maji, Kilimo, Uvuvi na hata Sekta ya uwekezaji ikiwemo kukuza sekta binafsi ili kuongeza upatikanaji wa ajira, haya anayafanya kwa nia iliyo njema kwa sababu ya upendo wake kwa wananchi."
Dkt.Mwigulu Nchemba anaendelea na ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi hapo kwa hapo jimboni humo.