Serikali yarekodi mafanikio tele Sekta ya Madini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde amesema, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, Sekta ya Madini nchini imeendelea kurekodi mafanikio makubwa.
"Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita tumeshuhudia mafanikio mbalimbali katika Sekta ya Madini ikiwemo kuendelea kuongezeka kwa mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa kutoka asilimia 6.7 mwaka 2020, asilimia 7.3 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 9.1 mwaka 2022.

Ameyasema hayo leo Aprili 30, 2024 wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma, hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Pia, amesema ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali uliongezeka kutoka shilingi 588,047,051,190.03 mwaka 2020/2021, shilingi 623,237,296,973.40 mwaka 2021/2022 hadi shilingi 678,042,598,813.92 mwaka 2022/2023.

Vile vile, Mheshimiwa Mavunde amesema, mafanikio mengine ni pamoja na kuongezeka kwa masoko na vituo vya ununuzi wa madini kutoka 41 na 61 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 42 na 100 mwaka 2023/2024 ambapo kulifanyika biashara ya madini yenye thamani ya shilingi 2,095,960,697,019.40 na shilingi 1,926,415,580,991.11 mtawalia.

"Aidha, Serikali imenunua mitambo mitano ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo na kuigawanya kwenye maeneo mbalimbali ya uchimbaji mdogo wa madini nchini."

Waziri Mavunde ameendelea kufafanua kuwa, ili kuendeleza Madini Muhimu na Madini Mkakati, Serikali imetoa leseni ya uchimbaji mkubwa wa madini Tembo (Heavy Mineral Sands) kwa mradi wa Tajiri uliopo Wilaya ya Pangani, Mkoa wa Tanga pamoja na Leseni ya Ujenzi wa Kiwanda cha Kusafisha Madini ya Metali Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga.

Biashara ya Madini

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mavunde akizungumzia kuhusu mwenendo wa biashaea ya madini duniani amesema,kwa kipindi cha kuanzia Julai, 2023 hadi Machi, 2024, bei ya madini ya dhahabu kwa wakia ilipanda hadi kufikia wastani wa dola za Marekani 2,138.01.

Hiyo ni ikilinganishwa na bei ya wastani wa dola za Marekani 1,854.54 katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023.

Amesema, kuongezeka kwa bei ya dhahabu kunatokana na sababu mbalimbali ikiwemo mahitaji makubwa ya madini hayo duniani.

"Kwa upande wa madini ya almasi, katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, mwenendo wa biashara ya madini hayo duniani umeendelea kusuasua kutokana na mdororo wa uchumi uliosababishwa na madhara ya vita kati ya Urusi na Ukraine."

Waziri Mavunde amesema, madini hayo yameshuka bei duniani kwa asilimia 19 kwa mwezi Machi, 2024.

Aidha, wastani wa mauzo ya madini ya almasi katika kipindi husika ni karati 201.71 yenye thamani ya dola za Marekani 43,231,183.71 ikilinganishwa na karati 271.74 yenye thamani ya dola za Marekani 50,824,739.77 katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi, 2023.

"Hatua zilizoanza kuchukuliwa na wazalishaji mbalimbali wa almasi duniani ni kupunguza uzalishaji wa almasi ili kuimarisha bei ya madini hayo.

"Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba nchi yetu ni miongoni mwa nchi zilizobarikiwa kuwa na madini mkakati ambayo uhitaji wake ni mkubwa kwenye nishati safi na salama na teknolojia nyingine za kisasa duniani."

Waziri Mavunde amesema, uhitaji huo unatokana na utekelezaji wa azimio la pamoja la Dunia la kupunguza hewa ya ukaa ifikapo 2050 (Net Zero Emission).

Miongoni mwa madini mkakati yanayopatikana nchini ni pamoja na lithium, cobalt, nikeli, shaba, aluminium, zinki, kinywe na rare earth elements (REE).

Amesema, ili nchi yetu iweze kunufaika na madini hayo,Wizara ya Madini imeandaa mkakati wa uendelezaji wa madini muhimu na madini mkakati hapa nchini.

"Mkakati huo unalenga kuhakikisha kwamba madini hayo yanaongezwa thamani hapa nchini ikiwemo kuzalisha bidhaa zinazohitajika katika soko kama vile betri za magari ya umeme na hivyo kuongeza manufaa kwa nchi ikiwemo kuongeza mapato ya Serikali na ajira kwa watanzania,"amebainisha Waziri Mavunde.

Wakati huo huo, Waziri Mavunde amesema, ili kuongeza manufaa yatokanayo na madini muhimu na madini mkakati, kwa mara ya kwanza kitajengwa kiwanda kikubwa na cha kisasa cha usafishaji na uongezaji thamani madini cha Multi Metals Processing Facility.

Ni katika eneo maalumu la ukanda wa kiuchumi la Buzwagi Special Economic Zone lililopo Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Ombi

Mheshimiwa Waziri Mavunde ameliomba Bunge liridhie na kupitisha makadirio ya shilingi 231,983,614,000.00 kwa ajili ya matumizi ya wizara na taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Kati ya fedha hizo shilingi 140,661,200,000.00 sawa na asilimia 60.63 ya bajeti yote ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Aidha, shilingi 91,322,414,000.00 sawa na asilimia 39.37 ya bajeti yote ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Huku kati ya fedha hizo, shilingi 24,872,875,000.00 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi (PE) na shilingi 66,449,539,000.00 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC) ya wizara na taasisi zilizo chini yake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news