DODOMA-Kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari kumechangia mafuriko ya mara kwa mara yanayoikumba mikoa ya Pwani na hivyo kusababisha mmomonyoko wa udongo na upotevu wa fukwe.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameliarifu Bunge jijini Dodoma leo Aprili 5, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Moshi Vijijini Prof. Patrick Ndakidemi aliyetaka kufahamu kama kuna ukweli kina cha maji ya Bahari ya Hindi nchini kimeongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi na nini athari zake.
Dkt. Jafo amesema kuwa kuongezeka kwa maji ya bahari kunasababishwa na kupanda kwa joto la dunia kutokana na kuendelea kuyeyuka kwa barafu katika maeno mbalimbali ya duniani.
Amesema kuwa utafiti na vipimo vilivyopo maji ya Bahari ya Hindi katika pwani ya Dar es Salaam unaeleleza kuwa maji yanaongezeka kwa wastani wa kiasi cha milimita 6 kwa mwaka tangu mwaka 2002.
Kwa mujibu wa Waziri Jafo, upotevu wa bioanuwai muhimu ikiwemo mikoko na nyasi bahari ambavyo ni sehemu ya hifadhi ya mazingira ni miongoni mwa madhara ya kuongezeka kwa kina cha bahari.
Ametaja madhara mengine kuwa kupotea kwa ardhi na kuwaacha wananchi bila ya makazi na kushindwa kufanya shughuli za kilimo kutokana na changamoto na changamoto ya kuongezeka kwa kiwango cha bahari.
Waziri Dkt. Jafo ameongeza kuwa visima vya maji baridi mbali na kuingiwa na maji ya chumvi pia miundombinu ikiwemo barabara, gati za bandari na majengo hubomolewa na maji hayo.
Kwa upande mwingine Waziri Jafo Serikali inaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kuzunguka Mlima Kilimanjaro ili kulinda barafu isipate changamoto.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Shally Raymond, Dkt. Jafo amepongeza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kuzalisha na kugawa miche kwa jamii ambayo inapandwa na kurejesha uoto wa asili.